YouVersion Logo
Search Icon

Danieli 12

12
Wakati wa mwisho
1 # Taz Mat 24:21; Marko 13:19; Ufu 7:14; 12:7 “ ‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa. 2#Taz Isa 26:19; Mat 25:46; Yoh 5:29 Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele. 3Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele. 4#Taz Ufu 22:10 Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”
5“Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili. 6Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe? 7#Taz Ufu 10:5; 12:14 Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’ 8Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’ 9Akanijibu, ‘Danieli, sasa nenda zako, kwani maneno haya ni siri na yamefungwa kwa kutiwa mhuri mpaka wakati wa mwisho. 10#Taz Ufu 22:11 Watu wengi wataondolewa uchafu, watatakaswa na kusafishwa. Lakini watu waovu wataendelea kutenda uovu. Hakuna hata mmoja wa hao waovu atakayeelewa; wenye hekima ndio watakaoelewa.
11 # Taz Dan 9:27; 11:31; Mat 24:15; Marko 13:14 “ ‘Tangu wakati wa kukomeshwa kwa sadaka za kuteketezwa kila siku, yaani kutoka wakati ule chukizo haribifu litakaposimamishwa itakuwa muda wa siku 1,290. 12Heri yao watakaostahimili mpaka siku zile 1,335 zitakapotimia.
13“ ‘Lakini wewe, ee Danieli, jiendee, ukapumzike kaburini, na wakati huo utakapotimia, utafufuka na kupata tuzo lako.’”

Currently Selected:

Danieli 12: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy