YouVersion Logo
Search Icon

Amosi 2

2
Moabu
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Moabu wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamemkosea heshima marehemu mfalme wa Edomu
kwa kuichoma moto mifupa yake
ili kujitengenezea chokaa!
2Basi, nitaishushia moto nchi ya Moabu,
na kuziteketeza kabisa ngome za mji wa Keriothi.
Wanajeshi watakapopaza sauti zao na kupiga tarumbeta,
watu wa Moabu watakufa katika makelele hayo ya vita.
3Isitoshe, nitamuua mtawala wa Moabu,
pamoja na viongozi wote wa nchi hiyo.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yuda
4Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Yuda wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamepuuza sheria zangu,
wala hawakufuata amri zangu.
Wamepotoshwa na miungu ileile waliyoihudumia wazee wao.
5Basi, nitaishushia moto nchi ya Yuda,
na kuziteketeza kabisa ngome za Yerusalemu.”
Hukumu ya Mungu juu ya Israeli
6Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Waisraeli wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamewauza watu waaminifu
kwa kuwa hawakuweza kulipa madeni yao;
na kuwauza watu fukara
wasioweza kulipa deni la kandambili.
7Huwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge,
na maskini huwabagua wasipate haki zao.
Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule,
hivyo hulitia unajisi jina langu takatifu.
8Popote penye madhabahu,
watu hulalia nguo walizotwaa kwa maskini
kama dhamana ya madeni yao;
na katika nyumba ya Mungu wao
hunywa divai waliyotwaa kwa wadeni wao.
9“Hata hivyo, enyi watu wangu,
kwa ajili yenu, niliwaangamiza kabisa Waamori
ambao walikuwa wakubwa kama mierezi,
wenye nguvu kama miti ya mialoni.
Naam, niliwaangamiza, matawi na mizizi.
10Niliwatoeni kutoka nchi ya Misri,
nikawaongoza kupitia jangwani miaka arubaini,
mpaka mkaichukua nchi ya Waamori kuwa yenu.
11Niliwateua baadhi ya wana wenu wawe manabii,
na baadhi ya vijana wenu wawe wanadhiri.
Je, enyi Waisraeli,
haya nisemayo si ya kweli?
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12Lakini nyinyi mliwafanya wanadhiri wanywe divai,
na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
13“Sasa basi, nitawagandamiza mpaka chini,
kama gari lililojaa nafaka.
14Hata wapiga mbio hodari hawataweza kutoroka;
wenye nguvu wataishiwa nguvu zao,
na askari watashindwa kuyaokoa maisha yao.
15Wapiga upinde vitani hawatastahimili;
wapiga mbio hodari hawataweza kujiokoa,
wala wapandafarasi hawatayanusurisha maisha yao.
16Siku hiyo, hata askari hodari
watatimua mbio bila chochote.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Currently Selected:

Amosi 2: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy