YouVersion Logo
Search Icon

Susana 1

1
1Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu aliyeishi Babuloni. 2Mtu huyo alioa mwanamke aliyeitwa Susana, binti Hilkia. Susana alikuwa mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. 3Wazazi wake walikuwa waadilifu na walimfunza binti yao kufuata sheria ya Mose. 4Yoakimu alikuwa mtu tajiri sana, na alikuwa na bustani kubwa karibu na nyumba yake. Kwa vile yeye alikuwa anaheshimika kuliko Wayahudi wote mjini humo, Wayahudi wenzake walikuwa wakijumuika nyumbani mwake kila wakati.
5Basi, mwaka huo, wazee wawili miongoni mwa jumuiya hiyo waliteuliwa kuwa waamuzi. Hao ndio wale ambao Bwana alisema juu yao: “Ufisadi utatokea huko Babuloni, kutoka kwa wazee waamuzi, ambao wanapaswa kuwaongoza watu!” 6Kila siku wazee hao walikuwa nyumbani kwa Yoakimu na mtu yeyote aliyekuwa na shtaka lake alilileta kwao.
7Basi, kila siku adhuhuri, wakati watu wote walipokuwa wameondoka Susana aliingia bustanini kwa mumewe kutembea. 8Wazee hao wawili walimwona akitembeatembea humo bustanini kila siku, nao wakaanza kumtamani. 9Walivutiwa na uzuri wake hata wakapoteza hamu ya kuomba wala kufikiria wajibu wao wa kutoa hukumu za haki. 10Wote walimtamani sana Susana, lakini kila mmoja wao hakumjulisha mwenzake shida yake. 11Kila mmoja aliona haya kumjulisha mwenzake kuwa alikuwa anamtamani kumpata yule mwanamke. 12Kila siku walikuwa wakichungulia kwa hamu kubwa ili mradi tu wamwone.
13Basi, siku moja adhuhuri wakaambiana; “Saa ya chakula imefika. Twende zetu nyumbani!” 14Basi, wakaondoka na kila mmoja akashika njia yake. Lakini kila mmoja akarudi nyuma. Mara wakakutana ana kwa ana. Walipoulizana kisa kila mmoja akakiri kuwa anamtamani Susana. Basi, wakaamua kwa pamoja kungojea wakati mzuri wa kumpata Susana akiwa peke yake.
15Ikawa nafasi waliyongojea ikapatikana: Susana aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake, akiwa ameandamana na watumishi wake wawili. Kwa vile kulikuwa na joto jingi siku hiyo, yeye alitaka kuoga humo bustanini. 16Kwa bahati nzuri, hapakuwa na mtu mwingine yeyote bustanini, ila tu wale wazee wawili waamuzi ambao walikuwa wamekaa chonjo mafichoni wakimvizia. 17Basi, Susana akawatuma watumishi wa kike nyumbani akisema, 18“Nendeni mkaniletee mafuta na marashi. Kisha fungeni milango ya bustani nipate kuoga.” Watumishi wa kike wakafanya kama walivyoambiwa; wakaifunga milango ya bustani na kupitia mlango wa pembeni kuchukua vitu walivyotumwa. Hawakuwaona wale wazee wawili waliokuwa wamejificha.
19Mara, wale watumishi wa kike walipotoka, wale wazee wawili wakajitokeza, wakamkimbilia Susana, 20wakamwambia, “Tazama, milango imefungwa, hivyo hakuna mtu atakayetuona. Sisi tunakupenda! Basi, tutimizie haja zetu. 21Ukikataa, tutakupeleka mahakamani na kutoa ushahidi kuwa ulikuwa na kijana fulani, ndiyo maana ukawaambia wale watumishi wa kike waende zao.”
22Susana alipiga kite, akasema, “Nimebanwa kila upande! Nikifanya mnalotaka, nitauawa; nikikataa, sitaweza kuokoka mikononi mwenu! 23Lakini afadhali mniue kuliko kufanya dhambi mbele ya Bwana.”
24Hapo, Susana akapiga kelele, nao wale wazee wawili wakampigia kelele. 25Mmoja wao akapiga mbio na kuifungua milango ya bustani. 26Watumishi wa nyumbani waliposikia makelele bustanini, wakakimbilia bustanini kwa kupitia mlango wa pembeni kuona yaliyompata Susana. 27Wale wazee wakamsingizia Susana kama walivyopanga. Wale watumishi wakaona aibu kubwa sana, maana Susana alikuwa hajawahi kupatikana na jambo kama hilo.
28Kesho yake, watu walipokusanyika tena nyumbani kwa Yoakimu, mumewe Susana, wale wazee wawili waamuzi walikuwapo pia. Walikuwa wamejizatiti kikamilifu kutekeleza njama zao ili Susana ahukumiwe adhabu ya kifo. 29Basi, wakasema mbele ya watu waliokuwa hapo, “Mwiteni Susana, binti Hilkia, mkewe Yoakimu.” 30Basi, watu wakaenda kumwita. Susana akaja, huku ameandamana na wazazi wake, mama yake na watoto wake, pamoja na ndugu zake wote. 31Susana alikuwa mwanamke mzuri na wa kupendeza sana. 32Alikuwa amejifunika shela usoni. Basi, waovu hao wawili wakaamuru shela liondolewe usoni ili wajishibishe kwa uzuri wake. 33Ndugu zake na wote waliomwona wakatokwa na machozi!
34Hapo, wale wazee wawili waamuzi wakasimama mbele ya watu wote, wakaiweka mikono yao juu ya kichwa cha Susana. 35Lakini yeye, huku machozi yanamchuruzika, akatazama juu mbinguni, maana, kwa moyo wake alimtumainia Bwana. 36Wale wazee wakasema, “Sisi, tulipokuwa tunatembeatembea bustanini peke yetu, mwanamke huyu aliingia ndani ya bustani pamoja na watumishi wa kike wawili, wakafunga milango ya bustani, kisha akawaruhusu waende zao. 37Punde si punde, kijana mmoja aliyekuwa amejificha, akatokea, akamwendea, akalala naye. 38Wakati huo wote, sisi tulikuwa pembeni mwa bustani. Tulishuhudia uovu wote huo, ndipo tukakimbilia mahali walipokuwa. 39Tuliwafumania wakikumbatiana. Lakini tulishindwa kumkamata yule kijana, kwani alituzidi nguvu; aliufungua mlango wa bustani, akatoroka. 40Lakini tulifaulu kumkamata huyu mwanamke. Na tulipomwuliza yule kijana ni nani, yeye alikataa kutuambia. Tunaapa kwamba hiyo ni kweli tupu.”
41Watu waliokusanyika mahali hapo wakawasadiki hao wazee wawili kwa vile wao walikuwa wazee wa watu tena ni waamuzi. Basi, wakamhukumu Susana auawe.
42Lakini Susana akalia kwa sauti kubwa, “Ee Mungu wa milele! Wewe waona yaliyofichika; wajua kila kitu hata kabla hakijatukia. 43Wewe wajua kwamba wazee hawa wananishuhudia uongo. Mimi sasa nitauawa. Lakini sikufanya hata mojawapo ya mambo wanayonisingizia!”
44Bwana akakisikia kilio cha Susana. 45Basi, alipokuwa anachukuliwa kwenda kuuawa, roho ya Mungu ikamchochea kijana mmoja aitwaye Danieli, 46akapiga kelele kwa sauti kubwa: “Mimi sihusiki na kifo cha mwanamke huyu!”
47Watu wote wakamgeukia, wakasema, “Unamaanisha nini kwa maneno hayo?” 48Danieli akajitokeza katikati yao, akasema, “Enyi Waisraeli! Je, mmekuwa wapumbavu kiasi hicho? Mtamhukumuje binti wa Israeli auawe bila kufanya uchunguzi na kupata ukweli wake? 49Rudini mahakamani. Wazee hawa wameshuhudia uongo dhidi ya Susana.”
50Basi, harakaharaka watu wakarudi nyumbani kwa Yoakimu. Wazee wakamwambia Danieli, “Haya kijana! Njoo uketi karibu nasi, utuambie hayo unayojua. Wewe ni kijana bado lakini Mungu amekujalia hekima!” 51Danieli akawaambia, “Watenganisheni hao waamuzi wawili, nami nitawahoji mmojammoja.”
52Walipotenganishwa, Danieli akamwita mmoja wao, akamwambia, “Wewe ni mzee lakini mwovu! Sasa utalipa kutokana na dhambi zako zote ulizotenda hapo awali. 53Wewe ulihukumu bila kutumia haki; asiye na hatia ukampatiliza na mwovu ukamwachilia. Ingawa Bwana alisema, ‘Mtu asiye na hatia, na mwenye haki, usimwue!’ 54Haya basi, kama kweli ulimwona waziwazi hebu: Niambie, walikuwa chini ya mti gani?” Mzee huyo akajibu, “Chini ya msandarusi.” 55Hapo Danieli akasema, “Barabara! Umejitia kitanzi kwa moyo wako mwenyewe! Sasa hivi malaika wa Mungu amekwisha pewa amri ya kukukata vipande viwili.”
56Kisha Danieli akamtoa huyo mzee, akaagiza yule mzee mwingine aletwe. Alipofika, Danieli akamwuliza, “Wewe ni mzawa wa Kanaani na si mzawa wa Yuda! Uzuri umekuhadaa mzee! Tamaa za mwili zimeupotosha moyo wako! 57Binti za Israeli wamekuwa wakitembea nawe kwa kuwa walikuogopa, lakini huyu binti wa Yuda hakukubaliana na uovu wako. 58Haya basi, hebu niambie: Walikuwa chini ya mti gani ulipowaona wakifanya mapenzi?” Naye akajibu, “Chini ya mwaloni.”#1:58 Msandarusi; mwaloni; mchezo wa maneno: Majina ya miti hiyo (54-55, 58-59) kwa Kigiriki yanafanana na maneno ya Kigiriki yanayotumika hapa “kukata” na “kuangamiza”. 59Danieli akasema, “Barabara! Nawe pia umejitia kitanzi kwa uongo wako mwenyewe. Malaika wa Mungu anakungoja mwenye upanga na atakukata vipande viwili. Nyote wawili mtaangamizwa.”
60Kisha, watu wote waliojumuika hapo wakapaaza sauti na kumsifu Mungu awaokoaye wenye kumtumainia. 61Basi, wakawavamia wale wazee wawili ambao Danieli alithibitisha uongo wa shtaka lao kwa maneno yao wenyewe. 62Kufuatana na sheria ya Mose, wanaotoa ushahidi wa uongo watapewa adhabu ileile ambayo aliyeshtakiwa angepewa. Basi, hao wazee wawili wakauawa na mama huyo asiye na hatia akaokolewa siku hiyo.
63Hilkia, baba yake Susana, mama yake, mumewe Yoakimu na ndugu zake, wakamsifu Mungu kwa sababu Susana hakupatikana na hatia yoyote dhidi ya shtaka hilo la aibu. 64Tangu siku hiyo, Danieli akaheshimika sana kati ya watu wake.

Currently Selected:

Susana 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy