Yeremia 6

6
Yerusalemu kuzingirwa na jeshi
1 “Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini!
Kimbieni kutoka Yerusalemu!
Pigeni tarumbeta katika Tekoa!
Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu!
Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini,
na uharibifu wa kutisha.
2 Nitamwangamiza Binti Sayuni,
aliye mzuri sana na mwororo.
3 Wachungaji pamoja na makundi yao
watakuja dhidi yake;
watapiga mahema yao kumzunguka,
kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”
4 “Jiandaeni kwa vita dhidi yake!
Inukeni tumshambulie mchana!
Lakini, ole wetu, mchana unaisha,
na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
5Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku,
na kuharibu ngome zake!”
6 Hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi:
“Kateni miti mjenge boma
kuzingira Yerusalemu.
Mji huu ni lazima uadhibiwe;
umejazwa na uonevu.
7 Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake,
ndivyo anavyomwaga uovu wake.
Ukatili na maangamizi vyasikika ndani yake,
ugonjwa wake na majeraha yake viko mbele yangu daima.
8 Pokea onyo, ee Yerusalemu,
la sivyo nitageukia mbali nawe
na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa,
asiweze mtu kuishi ndani yake.”
9Hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi:
“Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli
kwa uangalifu kama kwenye mzabibu;
pitisha mkono wako kwenye matawi tena,
kama yeye avunaye zabibu.”
10 Niseme na nani na kumpa onyo?
Ni nani atakayenisikiliza mimi?
Masikio yao yameziba#6:10 kwa Kiebrania masikio yao hayajatahiriwa,
kwa hiyo hawawezi kusikia.
Neno la Bwana ni chukizo kwao,
hawalifurahii.
11 Lakini nimejaa ghadhabu ya Bwana,
nami siwezi kuizuia.
“Wamwagie watoto walio barabarani,
na juu ya vijana wa kiume waliokusanyika;
mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake,
hata nao wazee waliolemewa na miaka.
12 Nyumba zao zitapewa watu wengine,
pamoja na mashamba yao na wake zao,
nitakapounyoosha mkono wangu
dhidi ya wale wanaoishi katika nchi,”
asema Bwana.
13 “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,
wote wana tamaa ya kupata faida zaidi;
manabii na makuhani wanafanana,
wote wanafanya udanganyifu.
14 Wanafunga majeraha ya watu wangu
bila uangalifu.
Wanasema, ‘Amani, amani,’
wakati hakuna amani.
15 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao
inayochukiza mno?
Hapana, hawana haya hata kidogo;
hawajui hata kuona aibu.
Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,
watashushwa chini nitakapowaadhibu,”
asema Bwana.
16 Hivi ndivyo asemavyo Bwana:
“Simama kwenye njia panda utazame,
ulizia mapito ya zamani,
ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo,
nanyi mtapata amani nafsini mwenu.
Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita njia hiyo.’
17 Niliweka walinzi juu yenu na kusema,
‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’
Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’
18 Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa,
angalieni, enyi mashahidi,
lile litakalowatokea.
19Sikia, ee nchi:
Ninaleta maafa juu ya watu hawa,
matunda ya mipango yao,
kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu
na wameikataa sheria yangu.
20 Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba,
au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?
Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki,
dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”
21 Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana:
“Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa.
Baba na wana wao watajikwaa juu yake,
majirani na rafiki wataangamia.”
22 Hivi ndivyo asemavyo Bwana:
“Tazama, jeshi linakuja
kutoka nchi ya kaskazini,
taifa kubwa linaamshwa
kutoka miisho ya dunia.
23 Wamejifunga pinde na mkuki,
ni wakatili na hawana huruma.
Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma
wanapoendesha farasi wao.
Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita
ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.”
24 Tumesikia taarifa zao,
nayo mikono yetu imelegea.
Uchungu umetushika,
maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
25 Usitoke kwenda mashambani
au kutembea barabarani,
kwa kuwa adui ana upanga,
na kuna vitisho kila upande.
26 Enyi watu wangu, vaeni magunia
mjivingirishe kwenye majivu,
ombolezeni kwa kilio cha uchungu
kama amliliaye mwana pekee,
kwa maana ghafula
mharibu atatujia.
27 “Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma,
nao watu wangu kama mawe yenye madini,
ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.
28 Wote ni waasi sugu,
wakienda huku na huko kusengenya.
Wao ni shaba na chuma,
wote wanatenda upotovu.
29Mivuo inavuma kwa nguvu,
kinachoungua kwa huo moto ni risasi,
lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure;
waovu hawaondolewi.
30 Wanaitwa fedha iliyokataliwa,
kwa sababu Bwana amewakataa.”

Zur Zeit ausgewählt:

Yeremia 6: NEN

Markierung

Kopieren

Vergleichen

Teilen

None

Möchtest du deine gespeicherten Markierungen auf allen deinen Geräten sehen? Erstelle ein kostenloses Konto oder melde dich an.