Yeremia 27
27
Yuda kumtumikia Nebukadneza
1 Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu#27:1 yaani Sedekia mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Tengeneza nira, ujivike shingoni mwako, uifunge kwa kamba za ngozi. 3Kisha utume ujumbe kwa wafalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni kupitia wajumbe ambao wamekuja Yerusalemu kwa Sedekia#27:3 yaani Yehoyakimu mfalme wa Yuda. 4Wape ujumbe kwa ajili ya mabwana zao na uwaambie: Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli: ‘Waambieni hivi mabwana zenu: 5Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooka nimeumba dunia na watu wake na wanyama walio ndani yake, nami humpa yeyote ninayependa. 6Sasa nitazitia nchi zenu zote mkononi mwa mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, na nitawafanya hata wanyama pori wamtumikie. 7Mataifa yote yatamtumikia yeye, pamoja na mwanawe, na mjukuu wake, hadi wakati wa nchi yake utakapowadia, kisha mataifa mengi na wafalme wenye nguvu nyingi watamshinda.
8“ ‘ “Lakini kama kukiwa na taifa lolote au ufalme ambao hautamtumikia Nebukadneza mfalme wa Babeli, ama kuinamisha shingo yake chini ya nira yake, nitaliadhibu taifa hilo kwa upanga, njaa na tauni, asema Bwana, hadi nitakapoliangamiza taifa hilo kwa mkono wake. 9Kwa hiyo msiwasikilize manabii wenu, waaguzi wenu, waota ndoto wenu, watabiri na wachawi wanaowaambia ninyi: Hamtamtumikia mfalme wa Babeli. 10Wanawatabiria uongo ambao utawafanya ninyi mhamishwe mbali kutoka nchi yenu. Nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia. 11Lakini ikiwa taifa lolote litainama na kuweka shingo yake katika nira ya mfalme wa Babeli na kumtumikia, nitaliacha taifa hilo katika nchi yake yenyewe ili wailime na kuishi humo, asema Bwana.” ’ ”
12 Nilitoa ujumbe huo huo kwa Sedekia mfalme wa Yuda. Nilisema, “Ingiza shingo yako katika nira ya mfalme wa Babeli, umtumikie yeye na watu wake, nawe utaishi. 13Kwa nini wewe na watu wako mfe kwa upanga, njaa na tauni, ambazo Bwana ameonya kuhusu taifa lolote ambalo halitamtumikia mfalme wa Babeli? 14Msiyasikilize maneno ya manabii wanaowaambia kwamba, ‘Hamtamtumikia mfalme wa Babeli,’ kwa sababu wanawatabiria uongo. 15‘Sikuwatuma hao,’ asema Bwana. ‘Wanatabiri uongo kwa jina langu. Kwa hiyo, nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia, ninyi pamoja na manabii wanaowatabiria.’ ”
16 Kisha nikawaambia makuhani na watu hawa wote, “Hili ndilo asemalo Bwana: Msiwasikilize manabii wanaosema, ‘Hivi karibuni sana vyombo vya nyumba ya Bwana vitarudishwa kutoka Babeli.’ Wanawatabiria ninyi uongo. 17Msiwasikilize. Mtumikieni mfalme wa Babeli, nanyi mtaishi. Kwa nini mji huu uwe magofu? 18Kama wao ni manabii na wanalo neno la Bwana, basi na wamsihi Bwana wa majeshi ili vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Bwana na katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda na katika Yerusalemu visipelekwe Babeli. 19Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi kuhusu zile nguzo, ile Bahari, vile vishikizo vinavyoweza kuhamishwa, vinara na vyombo vingine vilivyoachwa katika mji huu, 20ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli hakuvichukua alipomchukua Yekonia#27:20 au Konia; pia anaitwa Yehoyakini mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda kwenda uhamishoni huko Babeli kutoka Yerusalemu, pamoja na wakuu wote wa Yuda na Yerusalemu. 21Naam, hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu vitu ambavyo vimebaki ndani ya nyumba ya Bwana, na ndani ya jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, na katika Yerusalemu: 22‘Vitachukuliwa kupelekwa Babeli, na huko vitabaki hadi siku nitakayovijilia,’ asema Bwana. ‘Kisha nitavirudisha na kuvirejesha mahali hapa.’ ”
Zur Zeit ausgewählt:
Yeremia 27: NEN
Markierung
Kopieren
Vergleichen
Teilen
Möchtest du deine gespeicherten Markierungen auf allen deinen Geräten sehen? Erstelle ein kostenloses Konto oder melde dich an.
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.