Yeremia 20

20
Yeremia ateswa na Pashuri
1 Ikawa kuhani Pashuri mwana wa Imeri, mkuu wa maafisa wa Hekalu la Bwana, alipomsikia Yeremia akitoa unabii kuhusu mambo haya, 2akaamuru Yeremia nabii apigwe na kufungwa kwenye mkatale katika Lango la Juu la Benyamini katika Hekalu la Bwana. 3Siku ya pili Pashuri alipomwachia kwenye mkatale, Yeremia akamwambia, “Bwana hakukuita jina lako kuwa Pashuri bali Magor-Misabibu#20:3 maana yake Vitisho pande zote. 4Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nitakufanya uwe tisho kwako na rafiki wako wote; na macho yako mwenyewe yataona wakianguka kwa upanga wa adui zao. Nitawatia Yuda wote mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye atawachukua mateka na kuwapeleka Babeli, ama awaue kwa upanga. 5Nitatia utajiri wote wa mji huu kwa adui zao: yaani mazao yao yote, vitu vyao vyote vya thamani, na hazina zote za wafalme wa Yuda. Watavitwaa kwa nyara na kuvipeleka Babeli. 6Nawe Pashuri pamoja na wote wanaoishi katika nyumba yako mtaenda uhamishoni Babeli. Mtafia huko na kuzikwa, wewe na rafiki zako wote ambao umewatabiria uongo.’ ”
Malalamiko ya Yeremia
7 Ee Bwana, umenidanganya,
nami nikadanganyika;
wewe una nguvu kuliko mimi,
nawe umenishinda.
Ninadharauliwa mchana kutwa,
kila mmoja ananidhihaki.
8 Kila ninenapo, ninapiga kelele
nikitangaza ukatili na uharibifu.
Kwa hiyo neno la Bwana limeniletea matukano
na mashutumu mchana kutwa.
9 Lakini nikisema, “Sitamtaja
wala kusema tena kwa jina lake,”
neno lake linawaka ndani ya moyo wangu kama moto,
moto uliofungwa ndani ya mifupa yangu.
Nimechoka sana kwa kulizuia ndani mwangu;
kweli, siwezi kujizuia.
10 Ninasikia minongʼono mingi,
“Hofu iko pande zote!
Mshtakini! Twendeni tumshtaki!”
Rafiki zangu wote wananisubiri niteleze,
wakisema,
“Labda atadanganyika;
kisha tutamshinda
na kulipiza kisasi juu yake.”
11 Lakini Bwana yu pamoja nami
kama mpiganaji mwenye nguvu;
kwa hiyo watesi wangu watajikwaa,
Hawatashinda, nao wataaibika sana;
aibu yao haitasahaulika milele.
12 Ee Bwana wa majeshi,
wewe umjaribuye mwenye haki
na kupima moyo na nia,
hebu nione ukilipiza kisasi juu yao,
kwa maana kwako
nimeliweka shauri langu.
13 Mwimbieni Bwana!
Mpeni Bwana sifa!
Yeye huokoa uhai wa mhitaji
kutoka mikononi mwa waovu.
14 Ilaaniwe siku niliyozaliwa!
Nayo isibarikiwe ile siku
mama yangu aliyonizaa!
15Alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari,
yule aliyemfanya afurahi sana, akisema,
“Mtoto amezaliwa kwako,
tena mtoto wa kiume!”
16 Mtu huyo na awe kama ile miji ambayo
Bwana aliiangamiza bila huruma.
Yeye na asikie maombolezo asubuhi,
na ukelele wa vita adhuhuri.
17 Kwa sababu hakuniua nikiwa tumboni,
hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu,
nalo tumbo lake la uzazi
lingebaki kuwa kubwa daima.
18 Kwa nini basi nilitoka tumboni
ili kuona taabu na huzuni,
na kuzimaliza siku zangu katika aibu?

Zur Zeit ausgewählt:

Yeremia 20: NEN

Markierung

Kopieren

Vergleichen

Teilen

None

Möchtest du deine gespeicherten Markierungen auf allen deinen Geräten sehen? Erstelle ein kostenloses Konto oder melde dich an.