YouVersion 標識
搜索圖示

Mwanzo 1

1
Siku Sita Za Uumbaji Na Sabato
1 Hapo mwanzo Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mwenyezi Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
3 Mwenyezi Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mwenyezi Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mwenyezi Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mwenyezi Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
6 Mwenyezi Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8 Mwenyezi Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
9Mwenyezi Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mwenyezi Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mwenyezi Mungu akaona kuwa ni vyema.
11 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mwenyezi Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14 Mwenyezi Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mwenyezi Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mwenyezi Mungu akafanya nyota. 17Mwenyezi Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mwenyezi Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
20 Mwenyezi Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mwenyezi Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mwenyezi Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
24 Mwenyezi Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mwenyezi Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mwenyezi Mungu akaona kuwa hili ni jema.
26 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”
27 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mwenyezi Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31 Mwenyezi Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

目前選定:

Mwanzo 1: NMM

醒目顯示

分享

複製

None

想要在所有設備上保存你的醒目顯示嗎? 註冊或登入

YouVersion 使用 cookie 來個性化你的體驗。透過使用我們的網站,你即接受我們按照我們的 隱私政策所述來使用 cookie。