Waamuzi Utangulizi
Utangulizi
Jina la kitabu hiki limetokana na viongozi waliojulikana kama Waamuzi, ambao Mungu aliwainua kuongoza nchi ya Israeli. Hii ilitokana na kupotoka kwingi na kurudi nyuma kwa Waisraeli baada ya kifo cha Yoshua. Kwa sababu yeye alikuwa amewachagua kuwa watu wake, ambao kupitia kwao watu wote wangeweza kujua upendo wa Mungu, basi yeye hangewaacha wakandamizwe kabisa na adui zao. Kitabu hiki kinaelezea habari za Waisraeli kwa kipindi kati ya kifo cha Yoshua na huduma ya Samweli.
Mungu alikuwa amewasaidia Waisraeli kuishinda na kuiteka Kanaani, ambako ndani yake yaliishi mataifa mengi maovu. Waisraeli walikuwa katika hatari ya kuipoteza hii Nchi ya Ahadi kwa sababu walianza kumwasi Mungu. Walipomrudia Mungu, naye Mungu aliwainulia Waamuzi wa kuwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao, na kuwarudisha tena katika njia na kusudi lake, na kuwaongoza. Hivyo kipindi hiki kilijulikana kwa mashujaa walioitwa Waamuzi ambao waliyaongoza makabila ya Israeli. Jumla ya waamuzi kumi na wanne wameorodheshwa katika kitabu hiki kuwa waliiongoza Israeli. Wenye umaarufu zaidi walikuwa Yefta, Debora, Gideoni na Samsoni.
Mataifa yaliyowashambulia Waisraeli wakati wa kipindi hiki cha Waamuzi yalikuwa: Wakaldayo, Wamoabu, Wakanaani, Wamidiani, Waamoni na Wafilisti. Kipindi hiki cha Waamuzi kilidumu kwa miaka 410 kikitazamwa kwa namna matukio yalivyofuatana.
Mwandishi
Mwandishi wa kitabu hiki hajulikani ni nani, lakini mapokeo ya Kiyahudi yanasema ni Samweli.
Kusudi
Kuonesha kwamba hukumu ya Mungu juu ya dhambi ni lazima, na pia kuwasamehe na kuwarudisha waliotubu katika uhusiano wake ni lazima.
Mahali
Nchi ya Kanaani ambayo baadaye iliitwa Israeli.
Tarehe
Wakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani, lakini matukio yake ni mnamo 1375–1050 K.K.
Wahusika Wakuu
Othnieli, Ehudi, Debora, Gideoni, Abimeleki, Yefta, Samsoni na Delila.
Wazo Kuu
Baada ya Yoshua kufariki, Waisraeli waliongozwa na waamuzi. Walikuwa wakistawi walipompata kiongozi lakini baada ya kiongozi huyo kufariki walipotoka na kuangukia mikononi mwa adui zao. Walipomlilia Mungu aliwainulia mwamuzi, ambaye aliwaongoza na kuwapa ushindi.
Mambo Muhimu
Mambo mawili muhimu katika kitabu cha Waamuzi ni jinsi Waisraeli waligandamizwa na mataifa jirani kwa sababu ya kumwasi Mungu, na jinsi Mungu aliwakomboa kutoka kwa watesi wao baada ya kutubu na kumrudia.
Yaliyomo
Waisraeli kushindwa kuyafukuza kabisa mataifa yaliyokuwa nchi ya Kanaani (1:1–3:6)
Waamuzi wakomboa Waisraeli (3:7–16:31)
Waisraeli kuanguka kiroho, kimaadili na kisiasa (17:1–21:25).
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.