Walawi Utangulizi
Utangulizi
Kitabu cha Walawi kinajulikana kama “Kitabu cha Makuhani,” jina lililotokana na tafsiri ya Agano la Kale la Kiyunani. Walawi walichaguliwa na Mungu kuwa makuhani. Kitabu cha Walawi kina amri nyingi walizopaswa kuzitii na kuzitenda. Kazi ya ukuhani ilikuwa ya kushughulikia matatizo ya kila siku kuhusu uadilifu wa Waisraeli wote, jinsi ya kumwabudu Mungu, na kuishi katika utakatifu kama watu wateule wa Mungu.
Katika Agano la Kale, Mungu aliamuru kutolewa kwa sadaka na dhabihu, nazo zikapata maana kutokana na uhusiano wa Agano la Mungu na Israeli. Makusanyiko matakatifu yaliyofanyika katika mwaka yalitoa mwito kwa Waisraeli kufanya upya tabia na ile hali ya kutambua wajibu wao kama watu waliochaguliwa na Mungu. Ondoleo la dhambi lilifanyika kupitia kumwaga damu wakati wanyama walipokuwa wanatolewa dhabihu, kufuatana na maelekezo yaliyokuwa yametolewa kupitia kwa Musa.
Mwandishi
Musa.
Kusudi
Kuonesha kwa undani sheria zilizowaongoza Waisraeli, yaani makuhani pamoja na watu, katika agano la uhusiano na Mungu.
Mahali
Chini ya Mlima Sinai, wakati wa safari ya Waisraeli.
Tarehe
Mnamo 1450–1410 K.K.
Wahusika Wakuu
Walawi, Musa, Haruni (na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari), na Walawi wote.
Wazo Kuu
Kitabu hiki cha tatu miongoni mwa Vitabu Vitano vya Musa, kimsingi kinashughulikia jinsi ya kuishi maisha matakatifu na kumwabudu Mungu.
Mambo Muhimu
Utakatifu umetajwa mara nyingi katika kitabu hiki kuliko kitabu kingine chochote cha Biblia. Mungu anawafundisha Waisraeli jinsi ya kuishi maisha matakatifu: Mungu mtakatifu, ukuhani mtakatifu, watu watakatifu, dhabihu takatifu, vyombo vitakatifu, vyakula vitakatifu, pamoja na sheria ya utakatifu kwa ajili ya maisha ya utaua.
Yaliyomo
Amri na maelekezo ya kutoa dhabihu na sadaka (1:1–7:38)
Haruni na wanawe wateuliwa na Mungu kuwa makuhani (8:1–10:20)
Sheria zinazosimamia usafi na unajisi (11:1–15:33)
Siku ya Upatanisho (16:1‑34)
Sheria za utakatifu kimatendo (17:1–22:33)
Sikukuu zilizoamriwa, na mambo mengine (23:1–24:23)
Miaka maalum (25:1-55)
Mambo ya kufanya ili kustahili baraka za Mungu (26:1–27:34).
Selectat acum:
Walawi Utangulizi: NEN
Evidențiere
Copiază
Compară
Împărtășește
Dorești să ai evidențierile salvate pe toate dispozitivele? Înscrie-te sau conectează-te
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.