YouVersion Logo
Search Icon

Amosi 9

9
Adhabu ya Mungu
1Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama kando ya madhabahu, naye akaniamuru:
“Zipige hizo nguzo za hekalu
mpaka misingi yake itikisike.
Zivunje hizo nguzo ziwaangukie watu vichwani.
Wale watakaosalia nitawaua kwa upanga;
hakuna hata mmoja wao atakayenusurika,
naam, hakuna atakayetoroka.
2Wajapojichimbia njia ya kwenda kuzimu,
huko nitawachukua kwa mkono wangu;
wajapopanda mbinguni,
nitawaporomosha chini.
3Wajapojificha juu ya mlima Karmeli,
huko nitawasaka na kuwachukua;
wajapojificha mbali nami vilindini mwa bahari,
humo nitaliamuru joka la baharini liwaume.
4Wajapochukuliwa mateka na adui zao,
huko nitatoa amri wauawe kwa upanga.
Nitawachunga kwa makini sana
niwatendee mabaya na si mema.”
5Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
anaigusa ardhi nayo inatetemeka
na wakazi wake wanaomboleza;
dunia nzima inapanda na kushuka
kama kujaa na kupwa kwa mto Nili wa Misri.
6Mwenyezi-Mungu amejenga makao yake mbinguni,
nayo dunia akaifunika kwa anga;
huyaita maji ya bahari,
na kuyamwaga juu ya nchi kavu.
Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake!
Marekebisho baada ya uharibifu
7Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Kwangu mimi, nyinyi Waisraeli,
hamna tofauti yoyote na watu wa Kushi!#9:7 Kushi: Eneo ambalo sasa ni Ethiopia na sehemu ya Sudani.
Niliwatoa Wafilisti kutoka Krete,
na Waashuru kutoka Kiri,
kama nilivyowatoa nyinyi kutoka Misri.
8Mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nautazama ufalme wenye dhambi,
na nitauangamiza kabisa kutoka duniani.
Lakini sitawaangamiza wazawa wote wa Yakobo.
9“Tazama, nitatoa amri,
na kuwapepeta Waisraeli kati ya mataifa
kama mtu achekechavyo nafaka
niwakamate wote wasiofaa.
10Wenye dhambi miongoni mwa watu wangu,
watafia vitani kwa upanga;
hao ndio wasemao:
‘Maafa hayatatukumba wala kutupata!’
11“Siku yaja nitakapoisimika nyumba ya Daudi iliyoanguka;
nitazitengeneza kuta zake,
na kusimika upya magofu yake.
Nitaijenga upya kama ilivyokuwa hapo zamani.
12Nao Waisraeli watamiliki mabaki ya Edomu
na mataifa yote yaliyokuwa yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema,
na nitafanya hivyo.
13“Wakati waja kwa hakika,
ambapo mara baada ya kulima
mavuno yatakuwa tayari kuvunwa;
mara baada ya kupanda mizabibu
utafuata wakati wa kuvuna zabibu.
Milima itabubujika divai mpya,
navyo vilima vitatiririka divai.
14Nitarekebisha hali ya watu wangu Waisraeli.
Watajenga miji yao iliyoharibiwa na kuishi humo;
watapanda mizabibu na kunywa divai yake;
watalima mashamba na kula mazao yake.
15Nitawasimika katika nchi yao,
wala hawatang'olewa tena
kutoka katika nchi niliyowapa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Currently Selected:

Amosi 9: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy