YouVersion Logo
Search Icon

Barua ya Yeremia 1

1
1Hii ni nakala ya barua ambayo Yeremia aliwapelekea Waisraeli, muda mfupi tu kabla ya kuchukuliwa kwao mateka huko Babuloni na mfalme wa Babuloni. Barua yenyewe ina ujumbe ambao Mungu alimwamuru Yeremia awatangazie watu.
Uhamishoni muda mrefu
2Kwa sababu ya dhambi mlizomtendea Mungu, sasa mfalme Nebukadneza atawachukua mateka Babuloni. 3Baada ya kuwasili, mtabaki huko kwa muda wa miaka mingi; naam, kwa muda wa vizazi saba. Lakini baadaye, Mungu atawatoeni humo mje nyumbani kwa amani.
4Huko Babuloni, mtajionea wenyewe miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu na miti; miungu ambayo hubebwa mabegani na watu na kuwatia hofu watu wasiomjua Mungu. 5Jihadharini sana, msije mkaiga mitindo ya hao watu wa mataifa ya kigeni. Miungu hiyo isiwatie hofu mtakapowaona watu wakiiabudu katika maandamano yao. 6Ila, jisemeeni moyoni: “Wewe peke yako, ee Bwana, ndiwe tunayepaswa kukuabudu!” 7Malaika wa Mungu yu pamoja nanyi; yeye atawalinda.
Miungu ya uongo haina nguvu
8Kwa kweli, miungu hiyo inayo midomo, lakini imechongwa na mafundi; kweli imepakwa dhahabu na fedha, lakini si miungu ya kweli na haiwezi kuongea. 9Watu hao hutengeneza taji za dhahabu na kuivisha miungu hiyo kichwani, sawa na vile wamfanyiavyo msichana apendaye johari. 10Hutokea pia kwamba makuhani wao huiba kwa siri fedha na dhahabu hiyo, kwa matumizi yao wenyewe; 11tena hata huwapa malaya wa hekalu dhahabu na fedha hiyo. Miungu hiyo ya fedha, dhahabu na miti, huvishwa mavazi kana kwamba ni binadamu; 12lakini haiwezi kujiepusha na kutu au kuliwa na mchwa. 13Vumbi ya hekalu ikiangukia usoni, watu hulazimika kuipangusa. 14Miungu hiyo hushika mikononi fimbo ya kifalme, lakini haina uwezo wowote wa kumwangamiza anayeikosea. 15Hushika sime na shoka mikononi mwao, lakini haiwezi kujilinda vitani au dhidi ya wanyang'anyi. 16Hiyo hudhihirisha kwamba hiyo miungu si miungu ya kweli. Basi, msiiogope!
17Kama vile chungu kilichopasuka, ndivyo ilivyo hiyo miungu ya watu wasiomjua Mungu, miungu iliyowekwa mahekaluni; macho yao yamejaa vumbi linalotifuliwa na watu waingiao hekaluni. 18Na kama vile anavyofungwa mtu anayekabiliwa na hukumu ya kifo kwa kumkosea mfalme, ndivyo makuhani wanavyolinda mahekalu ya miungu hiyo kwa malango yenye makufuli na makomeo ya chuma ili kujikinga na wanyang'anyi. 19Miungu hiyo huwashiwa taa nyingi kuliko wanavyohitaji wenyewe, lakini haiwezi kuona chochote. 20Inafanana na mojawapo ya maboriti ya hekalu yaliyogugunwa toka ndani na mchwa iliyotoka ardhini na kuyala na kuharibu pia mavazi yao mazuri. Lakini yenyewe haina habari hata kidogo. 21Nyuso zao zimekuwa nyeusi kutokana na moshi hekaluni. 22Popo, mbayuwayu na ndege wengineo hurukaruka na kutua juu ya miili yao na vichwa vyao; hata paka huikalia. 23Hayo yote yatawadhihirishieni kwamba hiyo si miungu ya kweli. Basi, msiiogope!
24Na, kuhusu hiyo dhahabu ambayo hiyo miungu imepakwa kuifanya ipendeze, dhahabu yenyewe isiposuguliwa na mtu, haiwezi kung'aa. Ilipokuwa inatengenezwa, yenyewe haikuhisi chochote! 25Hata ikinunuliwa kwa fedha ya thamani kubwa kiasi gani, haiwezi kabisa kupumua. 26Hubebwa na watu mabegani kwa sababu haiwezi kutembea kwa miguu yake yenyewe. Hiyo inaonesha watu wazi kwamba haina faida yoyote. 27Hata hao wanaoihudumia huionea aibu wakati inapoanguka chini, maana hulazimika kuinuliwa tena. Mtu akiisimamisha mahali fulani haiwezi kusogea, na ikikaa kombo haiwezi kujisimamisha wima. Kuipa zawadi ni sawa na kumpa maiti! 28Makuhani huchukua matambiko yaliyotolewa kwa hiyo miungu na kuyauza kwa faida yao, na wake zao huhifadhi sehemu ya matambiko hayo kwa kuyatia chumvi, badala ya kuwagawia maskini na wasiojiweza. 29Hata wanawake walio katika hedhi na waliojifungua karibuni huruhusiwa kugusa matambiko hayo. Mambo hayo yawahakikishieni kwamba hiyo si miungu. Basi, msiiogope!
30Basi, itaitwaje miungu, hali wanawake#6:30 wanawake: Huko Israeli haikuruhusiwa wanawake kuwa makuhani. ndio wanaoitumikia miungu hiyo ya fedha, dhahabu na miti? 31Hata makuhani hufanya maombolezo yao huko hekaluni wakiwa wamevaa mavazi yaliyotatuka, wamenyoa nywele zao na vichwa wazi. 32Makuhani hao hupaaza sauti na kupiga kelele mbele ya miungu yao kama watu wafanyavyo kwenye karamu za matanga. 33Baadhi yao huchukua mavazi ya miungu hiyo na kuwavisha wake zao na watoto wao. 34Kuitendea miungu hiyo mema au mabaya si neno; yenyewe haiwezi kujilipiza kisasi. Haiwezi kutawaza mfalme wala kumwondoa madarakani. 35Hali kadhalika haiwezi kumpa mtu utajiri au fedha. Mtu akiiwekea nadhiri, lakini asiitimize, miungu hiyo haiwezi kumdai aitimize. 36Haiwezi kamwe kumwokoa mtu katika kifo, wala kumlinda mtu dhaifu dhidi ya mwenye nguvu. 37Haiwezi kamwe kumjalia kipofu kuona wala kumwondoa mtu taabuni. 38Haiwezi kuwahurumia wajane au kuwasaidia yatima. 39Madude haya yaliyotengenezwa kwa miti na kupakwa fedha na dhahabu ni kama mawe tu yaliyochongwa kutoka milimani; watu waitumikiao wataaibika. 40Watu wanawezaje, basi, kuifikiria kuwa miungu au kuiita miungu?
Upumbavu wa kuabudu sanamu
Licha ya hayo, hata Wakaldayo wenyewe huidharau miungu hiyo yao. 41Ikiwa mtu ni bubu, wao humpeleka hekaluni mbele ya Beli na kumwomba amwezeshe kuongea, kana kwamba mungu Beli ana kipawa cha kufahamu chochote. 42Watu hao hawawezi kufikiri kiasi cha kutosha kuamua kuachana na hiyo miungu isiyo na akili. 43Isitoshe, wanawake hujifunga mishipi na kukaa barabarani wakijifukizia ubani na kufanya umalaya wao. Mmoja wao akichukuliwa na mwanamume na kulala naye, hurudi na kumcheka mwenziwe aliyebaki, eti kwamba si mzuri kama yeye, ndio maana hakuchaguliwa. 44Kila kitu kuhusu miungu hiyo ni uongo mtupu; yawezekanaje, basi, kuifikiria au kuiita miungu?
45Miungu hiyo imetengenezwa na maseremala na wafua dhahabu; haiwezi, basi, kuwa kitu kingine mbali na kile ambacho mafundi hao walitaka iwe. 46Hata hao walioitengeneza wenyewe hawaishi muda mrefu! Yawezekanaje basi, vitu hivyo walivyotengeneza watu hao kuwa miungu? 47Hivyo ndivyo watu wanavyowaachia wazawa wao uongo na aibu. 48Vita au balaa likitokea, makuhani hushauriana wao kwa wao watajificha wapi pamoja na miungu yao hiyo. 49Vitu hivyo haviwezi kujiokoa vyenyewe wakati wa vita au balaa lifikapo. Kwa nini, basi, watu hawawezi kutambua kwamba sanamu hizo si miungu?
50Miungu hiyo ni vitu tu vilivyotengenezwa kwa miti, vikapakwa dhahabu na fedha. Zaidi ya hayo, itadhihirika siku moja kwamba yote ni uongo mtupu. 51Mataifa yote na wafalme watatambua kwamba sanamu hizo si miungu, ila ni vitu tu vilivyotengenezwa kwa mikono ya wanaadamu. Ndani yake hamna utendaji wowote wa Mungu. 52Nani, basi, asiyeweza kukubali kwamba sanamu hizo si miungu?
53Hiyo miungu haiwezi kumtawaza mfalme wala kuwapa watu mvua. 54Haiwezi kutoa kauli juu ya mambo yao yenyewe wala kumsaidia mtu aliyedhulumiwa; haiwezi kabisa kufanya lolote; ni kama kunguru tu wanaorukaruka angani. 55Patokeapo moto hekaluni, makuhani hutimua mbio kujisalimisha, huku miungu iliyotengenezwa kwa miti na kupakwa fedha na dhahabu huachwa ikateketea kama maboriti. 56Isitoshe, haiwezi hata kupingana na mfalme wala kupigana na adui. Yawezekanaje, basi, kuamini au kuifikiria hiyo kuwa miungu?
Udhaifu wa miungu ya uongo
57Miungu ya miti iliyopakwa fedha na dhahabu haiwezi kujikinga na wezi au wanyang'anyi 58ambao huiba fedha na dhahabu na kujiendea zao, huku wamechukua pia mavazi iliyovishwa. Naam, haiwezi kujilinda kabisa! 59Afadhali mfalme hodari au chombo cha matumizi nyumbani kinachomfaa mwenyewe, kuliko miungu hii ya uongo. Hata afadhali mlango wa nyumba ambao hulinda vitu vilivyomo nyumbani, kuliko hiyo miungu ya uongo. Nguzo moja ya mti katika ikulu ya mfalme ni bora kuliko hiyo miungu ya uongo.
60Jua, mwezi na nyota, hutii na kutoa mwanga kufuata mwongozo wa Mungu. 61Hali kadhalika umeme na upepo. Umeme utokeapo huonekana kwa urahisi kila mahali, nao upepo huvuma pande zote. 62Mungu anapoamuru mawingu kutanda juu ya dunia yote, mawingu hutekeleza amri yake. 63Mungu anapoteremsha moto kutoka mbinguni kuteketeza milima na misitu, moto hutii amri hiyo. Lakini sanamu za miungu ya uongo haziwezi kufanya mambo hayo, haziwezi hata kuiga mambo hayo. 64Kutokana na hayo, na kwa vile haziwezi kumhukumu mtu wala kumfaa, haziwezi kamwe kufikiriwa kuwa ni miungu. 65Basi, nyinyi mwajua kwamba sanamu hizo si miungu. Kwa hiyo, msiziogope!
66Kwa kweli, miungu hiyo haiwezi kuwalaani wafalme wala kuwabariki. 67Haiwezi kuyafanyia mataifa ishara angani; haiwezi kuangaza kama jua au mwezi. 68Hata wanyama wa porini ni bora kuliko hizo sanamu za miungu maana wao wanaweza angalau kukimbia hatari ili kujiokoa. 69Basi, kwa vyovyote vile, hakuna ushahidi wowote kwamba hiyo ni miungu. Kwa hiyo, msiiogope hata kidogo!
70Hizo sanamu za miungu zilizotengenezwa kwa miti na dhahabu na fedha, ni kama kinyago cha kufukuzia kunguru katika shamba la matango. Haziwezi kumlinda mtu yeyote. 71Kadhalika, miungu hiyo ya miti iliyopakwa dhahabu na fedha ni kama kichaka bustanini; badala ya kuwazuia ndege wasije bustanini, huwapatia ndege hao mahali pa kutua. Naam, ni kama mzoga uliotupwa gizani. 72Mavazi ya kitani ya zambarau na mng'ao wake huozea juu ya miungu hiyo; hivyo mtatambua kwamba, hiyo si miungu hata kidogo. Hatimaye, huliwa na mchwa na kuwa kitu cha kudharauliwa nchini. 73Basi, afadhali mtu mwadilifu asiye na sanamu za miungu; huyo hatadharauliwa.

Currently Selected:

Barua ya Yeremia 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy