Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 52:1-10

Isaya 52:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Amka, amka, ee Sayuni, jivike nguvu. Vaa mavazi yako ya fahari, ee Yerusalemu, mji mtakatifu. Asiyetahiriwa na aliye najisi hataingia kwako tena. Jikungʼute mavumbi yako, inuka, uketi kwenye kiti cha utawala, ee Yerusalemu. Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako, ee Binti Sayuni uliye mateka. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: “Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.” Kwa maana hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi, hatimaye, Ashuru wakawadhulumu. “Basi sasa nina nini hapa?” asema BWANA. “Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo, nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,” asema BWANA. “Mchana kutwa jina langu limetukanwa bila kikomo. Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu; kwa hiyo katika siku ile watajua kwamba ndimi niliyetangulia kulisema. Naam, ni mimi.” Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema ilivyo mizuri juu ya milima, wale wanaotangaza amani, wanaoleta habari njema, wanaotangaza wokovu, wauambiao Sayuni, “Mungu wako anatawala!” Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao, pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha. BWANA atakaporejea Sayuni, wataliona kwa macho yao wenyewe. Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja, enyi magofu ya Yerusalemu, kwa maana BWANA amewafariji watu wake, ameikomboa Yerusalemu. Mkono mtakatifu wa BWANA umefunuliwa machoni pa mataifa yote, nayo miisho yote ya dunia itaona wokovu wa Mungu wetu.

Shirikisha
Soma Isaya 52