Isaya 24:16-23
Isaya 24:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Tunasikia nyimbo za sifa kutoka miisho ya dunia, nyimbo za kumsifu Mungu aliye mwadilifu. Lakini mimi ninanyongonyea, naam, ninanyongonyea. Ole wangu mimi! Wasaliti wanaendelea kuwa wasaliti, usaliti wao unazidi kuwa mbaya zaidi. Hofu, mashimo na mitego, hivi ndivyo vinavyowangojeni enyi wakazi wa dunia. Atakayeikimbia hofu atatumbukia shimoni; atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni. Madirisha ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia inavunjikavunjika, inapasuka na kutikiswatikiswa. Inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda. Imelemewa na mzigo wa dhambi zake nayo itaanguka wala haitainuka tena. Siku ile Mwenyezi-Mungu ataliadhibu jeshi la angani kadhalika na wafalme wa duniani. Wote watakusanywa kama wafungwa shimoni; watafungwa gerezani pamoja kwa miaka mingi, na baada ya muda huo atawaadhibu. Kisha mwezi utaaibishwa, nalo jua litaona aibu kuangaza, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatawala huko Yerusalemu katika mlima Siyoni; ataonesha wazee wa watu wake utukufu wake.
Isaya 24:16-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, viko juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewalewa kama mlevi, nayo inawayawaya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena. Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi wataadhibiwa. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Isaya 24:16-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena. Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Isaya 24:16-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!” Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani. Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa. Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena. Katika siku ile BWANA ataadhibu mamlaka zilizo juu mbinguni, na wafalme walio chini duniani. Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani; watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi. Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana BWANA wa majeshi atatawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake, kwa utukufu.