Mwanzo 33:1-11
Mwanzo 33:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yakobo alitazama, akamwona Esau akija pamoja na watu 400. Hapo, akawagawa watoto wake kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wawili. Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Raheli na mwanawe Yosefu. Kisha yeye mwenyewe akawatangulia, akaenda akiinama mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake. Basi, Esau akaenda mbio kumlaki Yakobo, akamkumbatia na kumbusu shingoni, na wote wawili wakalia. Esau alipotazama na kuwaona wale kina mama na watoto, akauliza, “Ni kina nani hawa ulio nao?” Yakobo akamjibu, “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mtumishi wako.” Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima. Hali kadhalika Lea akaja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Hatimaye, Raheli na Yosefu wakaja, wakainama kwa heshima. Ndipo Esau akauliza, “Nini maana ya kundi hili nililokutana nalo njiani?” Yakobo akamjibu, “Nilitumaini kupata fadhili kwako ee bwana wangu.” Lakini Esau akasema, “Nina mali ya kutosha ndugu yangu. Mali yako na iwe yako mwenyewe.” Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa. Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.
Mwanzo 33:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao. Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho. Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililokutana nalo, maana yake ni nini? Akasema, Ili kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, hifadhi uliyo nayo yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; nakuomba kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, Hakika, kuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu – maana umenipokea kwa kibali kama chake. Tafadhali pokea zawadi yangu iliyoletwa kwako, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote. Akamsihi sana, naye akapokea.
Mwanzo 33:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao. Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho. Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea.
Mwanzo 33:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yakobo akainua macho, akamwona Esau akija na watu wake mia nne. Kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale wajakazi wake wawili. Akawaweka wale wajakazi na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, nao Raheli na Yusufu wakaja nyuma. Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu hadi chini mara saba alipomkaribia ndugu yake. Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia. Esau akainua macho, akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa waliofuatana nawe ni nani?” Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.” Kisha wale wajakazi na watoto wao wakakaribia na kusujudu. Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yusufu na Raheli, nao pia wakasujudu. Esau akauliza, “Makundi hayo yote niliyokutana nayo yana maana gani?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.” Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.” Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa kibali kikubwa. Tafadhali kubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.