Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 1:26-56

Luka 1:26-56 BHN

Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!” Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake. Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea. Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti. Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu, akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.” Naye Maria akasema, “Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu, jina lake ni takatifu. Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake, kama alivyowaahidia wazee wetu, Abrahamu na wazawa wake hata milele.” Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.