Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 13

13
Yesu awaosha wanafunzi miguu
1 # Yn 7:30; 8:20; 15:13; Gal 2:20; 1 Yoh 3:16 Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, huku akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye akiwa amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. 2#Lk 22:3 Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, moyo wa kumsaliti; 3#Yn 3:35; 16:28; 17:2 Yesu, huku akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, 4#Mt 11:29; 20:28; Lk 12:37 aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. 5Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. 6#1 Pet 5:3 Akamfikia Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe waniosha miguu mimi? 7Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. 8#Yn 13:12 Petro akamwambia, Wewe hutaniosha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Nisipokuosha, huna shirika nami. 9Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. 10#Yn 15:3 Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga mwili#13:10 Katika Kigiriki hakuna neno mwili. hana haja ila ya kuosha miguu, maana yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. 11#Yn 6:64,70,71 Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi.
12 # Lk 22:27 Basi alipokwisha kuwaosha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa hayo niliyowatendea? 13#Mt 23:8,10 Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. 14#Lk 22:27; 1 Tim 5:10 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha miguu, imewapasa ninyi pia kuoshana miguu ninyi kwa ninyi. 15#Flp 2:5; Kol 3:13; 1 Pet 2:21 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. 16#Mt 10:24; Lk 6:40; Yn 15:20 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyemtuma. 17#Mt 7:24; Yak 1:25 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. 18#Zab 41:9 Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa,
Aliyekula chakula changu
Ameniinulia kisigino chake.
19 # Yn 14:29 Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye. 20#Mt 10:40; Mk 9:37; Lk 9:48; 10:16 Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu yeyote nimtumaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi; ampokea yeye aliyenituma.
Yesu atabiri juu ya kusalitiwa kwake
21 # Mt 26:21-25; Mk 14:18-21; Lk 22:21-23 Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. #Yn 12:27 22Wanafunzi wakatazamana, huku wakiwa na mashaka ni nani amnenaye. 23#Yn 19:26; 20:2; 21:7,20 Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. 24Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? 25Basi yeye, huku akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? 26Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. 27#Yn 13:2 Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. 28Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. 29#Yn 12:6 Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. 30Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.
Amri mpya
31Basi huyo alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32#Yn 12:23; 17:1-5 Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. 33#Yn 7:34; 8:21 Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi. 34#Yn 15:12,13,17; Yn 3:23; 2 Yoh 1:5; 1 Yoh 2:8,10 Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. 35Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.
Yesu atabiri kuwa Petro atamkana
36 # Mt 26:33-35; Mk 14:29-31; Lk 22:31-34 Simoni Petro akamwambia, Bwana, unakwenda wapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye. #Yn 7:34; 21:18,19 37Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako. 38Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jogoo hatawika hadi wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 13: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha