Yoshua Mwana wa Sira 41
SRUVDC

Yoshua Mwana wa Sira 41

41
Kuhusu Kifo
1Ewe Mauti!
Ukumbusho wako ni uchungu!
Kwake akaaye na amani katika kikao chake,
Asiye na neno la kumfadhaisha;
Ambaye amefanikiwa katika yote,
Naye ana nguvu ya kula anasa.
2Ewe Mauti!
Hukumu yako ina kibali!
Kwake aliye fukara, amepungukiwa na nguvu,
Mwenye miaka mingi, naye mzee sana;
Ambaye aona fadhaa juu ya mambo yote,
Naye ni mkaidi, ametindikiwa na saburi.
3Usiogope hukumu ya mauti;
Uwakumbuke waliotangulia,
Na wale watakaofuata.
4Ndiyo hukumu ya BWANA juu ya wote;
Mbona wewe unakataa?
Ndiyo mapenzi yake Aliye Juu,
Kama ni miaka kumi,
Au mia, au miaka elfu,
Hakuna kuhoji wingi wa siku kaburini.
Ajali ya Mwovu
5Kizazi cha wakosaji ni makuruhi, nao huzoea kukaa katika nyumba za wahalifu. 6Urithi wa wana wa wakosaji utaharibika, na kwa wazao wao kutakuwapo shutumu la daima, 7Watoto watamnung'unikia baba aliye mwovu, madhali kwa ajili yake watalaumiwa.
8Ole wenu! Watu waovu,
Mlioiacha sheria ya Mungu Aliye Juu!
9Kuzaa mtazaa kwa madhara,
Na kuzaliwa mtazaliwa kwa kuugua;
Mkijikwaa, itawafurahisha watu,
Na mkifa, sehemu yenu itakuwa laana.
10Yote yaliyo ya ubatili yataurudia ubatili, kadhalika na waovu wataendelea kutoka laana hata Jehanamu. 11Wanadamu ni ubatili kwa habari ya miili yao; lakini jina la watauwa halitafutiwa mbali. 12Ujilinde sifa yako; maana itadumu kwako kuliko hazina elfu za thamani. 13Maisha mema yana siku zake; lakini sifa njema yadumu milele.
Haya
14Wanangu sikilizeni mafundisho juu ya haya, na kuona soni sawasawa na hukumu yangu; 15kwa maana si vema kuishika haya ya kila namna; 16pia si kila namna ya soni inayopendeza.
Adabu Maishani
17Basi, mambo haya uyatahayarikie; uzinifu mbele ya baba na mama; na uongo mbele ya mtawala na mkuu; 18ulaghai mbele ya bwana na bibi; na dhambi mbele ya mkutano wa watu; 19Udhalimu mbele ya mshiriki na rafiki; na kiburi mahali ukaapo kama mgeni; 20na kubadili kiapo na agano; kujiegama juu ya kiwi chakulani; 21kumkataa kwa dharau mtu aombaye bakshishi; kugeuza uso wako mbali na jamaa yako; kuuzuia bila haki mgawanyo wa urithi; kunyamaza kwao wanaokusalimu; 22kumtazama mwanamke aliye malaya; 23kumkodolea macho mwanamke aliyeolewa; 24kujishughulisha mno na mjakazi wake, wala usikaribie kitanda chake; 25makaripio mbele ya rafiki, na mashutumu ukiisha kumfadhili mtu; 26kumwambia mtu mwingine neno ulilolisikia, na kufunua siri. 27Hivyo utakuwa mwenye haya kweli kweli, na kuona kibali machoni pa kila mtu aliye hai.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Jifunze Mengi Kuhusu Swahili Revised Union Version