Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 19:1-16

Ufunuo 19:1-16 NENO

Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipaza sauti na kusema: “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu, kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.” Wakasema tena kwa sauti kuu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.” Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!” Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!” Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipaza sauti na kusema: “Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari. Akapewa kitani safi, inayongʼaa na nzuri, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.) Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndio maneno ya kweli ya Mungu.” Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.” Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. Amevaa joho lililoloweshwa katika damu, na Jina lake ni Neno la Mungu. Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili: Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.