Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 2:1-40

Luka 2:1-40 NENO

Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi. (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.) Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa. Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito. Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia, naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni. Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote. Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo, Bwana. Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ngʼombe.” Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.” Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona. Hata zilipotimia siku nane, uliokuwa wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilopewa na malaika kabla hajatungwa mimba. Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Sheria ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”. Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema: “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi, sasa mruhusu mtumishi wako aende kwa amani. Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako, ulioweka tayari machoni pa watu wote, nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.” Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.” Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu. Yusufu na Mariamu walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya. Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akijawa na hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.