Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 1:26-56

Luka 1:26-56 NENO

Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yusufu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Mariamu. Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!” Mariamu akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni salamu hii ni ya namna gani. Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu; umepata kibali kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume na utamwita jina Yesu. Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha utawala cha Daudi baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Mariamu akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?” Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha. Wakati huo Mariamu akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye nchi ya vilima ya Yudea. Akaingia nyumbani mwa Zakaria na kumsalimu Elizabeti. Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, akapaza sauti kwa nguvu, akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. Lakini ni kwa nini mimi nimepata kibali kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliye tumboni mwangu aliruka kwa furaha. Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.” Naye Mariamu akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu, kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa, kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu. Rehema zake hudumu kizazi hadi kizazi, kwa wale wanaomcha. Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao. Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya utawala, lakini amewainua wanyenyekevu. Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu. Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.” Mariamu akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani mwake.