Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 30:8-18

Isaya 30:8-18 NENO

Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya BWANA. Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!” Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja. Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka. Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi wanaoenda kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza wataenda kasi! Watu elfu moja watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.” Hata hivyo BWANA anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonesha huruma. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!