Matendo 2:29-47
Matendo 2:29-47 NENO
“Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu wa zamani Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa hadi leo. Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo, kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha utawala. Daudi, akiona mambo yaliyo mbele, akanena kuhusu kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. Mungu alimfufua huyu Yesu, na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. Basi yeye ametukuzwa hadi mkono wa kuume wa Mungu, na amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema, “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.”’ “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.” Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?” Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.” Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa, na siku ile waliongezeka watu wapatao elfu tatu. Nao wakadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. Waumini wote walikuwa mahali pamoja, nao wakashirikiana katika mambo yote. Waliuza mali yao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.





