2 Yohana 1
1
Salamu
1 Mzee.
Kwa mama mteule na watoto wake, ninaowapenda katika kweli; wala si mimi tu, bali na wale wote wanaoijua kweli; 2kwa sababu ya ile kweli inayokaa ndani yetu, na ambayo itaendelea kukaa nasi milele.
3 Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.
Kweli na upendo
4Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza. 5Sasa, mama mteule mpendwa, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Tupendane kila mmoja na mwenzake. 6Hili ndilo pendo: kwamba tuenende kwa kuzitii amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.
7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametawanyika ulimwenguni. Mtu kama huyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo. 8Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu. 9Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo bali ameyaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. 10Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. 11Yeyote amkaribishaye mtu kama huyo anashiriki katika matendo yake maovu.
Salamu za mwisho
12 Ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kwenu na kuongea nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.
13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Amen.
Iliyochaguliwa sasa
2 Yohana 1: NEN
Kuonyesha
Nakili
Linganisha
Shirikisha
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.