Mathayo 5

5
Hotuba mlimani
1Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea, 2naye akaanza kuwafundisha:
Furaha ya kweli
(Luka 6:20-23)
3“Heri walio maskini rohoni,
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4Heri walio na huzuni,
maana watafarijiwa.
5 # Taz Zab 37:11 Heri walio wapole,
maana watairithi nchi.
6Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu,
maana watashibishwa.
7Heri walio na huruma,
maana watahurumiwa.
8 # Taz Zab 24:3-4 Heri wenye moyo safi,
maana watamwona Mungu.
9Heri wenye kuleta amani,
maana wataitwa watoto wa Mungu.
10Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu,
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11“Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
Chumvi na mwanga
Marko 9:50; Luka 14:34-35
13“Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu.
14“Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. 15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. 16Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Kuhusu sheria
17“Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha. 18Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia. 19Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. 20Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Kuhusu hasira
(Luka 12:57-59)
21“Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’ 22Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.
23“Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe, 24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako.
25“Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani. 26Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho.
Kuhusu uzinzi
27“Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’ 28Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake. 29Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, lingoe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu. 30Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.
Kuhusu talaka
(Mat 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18)
31“Ilikwisha semwa pia: ‘Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka’. 32Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mwanamume akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.
Kuhusu kiapo
33“Tena mmesikia kwamba watu wa kale waliambiwa: ‘Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’ 34Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; 35#Taz Zab 48:2 wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. 36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37Ukisema, ‘Ndiyo’, basi iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.
Kuhusu kulipiza kisasi
(Luka 6:29-30)
38“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ 39Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili. 40Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. 41Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. 42Akuombaye mpe, wala usimpe kisogo anayetaka kukukopa kitu.
Kuwapenda maadui
(Luka 6:27-28,32-36)
43“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako, na kumchukia adui yako.’ 44Lakini mimi nawaambieni, wapendeni maadui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyinyi, 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu. 46Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda nyinyi? Hakuna! Kwa maana, hata watozaushuru hufanya hivyo! 47Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo. 48Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Выбрано:

Mathayo 5: BHND

Выделить

Поделиться

Копировать

None

Хотите, чтобы то, что вы выделили, сохранялось на всех ваших устройствах? Зарегистрируйтесь или авторизуйтесь

YouVersion использует файлы cookie, чтобы персонализировать ваше использование приложения. Используя наш веб-сайт, вы принимаете использование нами файлов cookie, как описано в нашей Политике конфиденциальности