YouVersion Logo
Search Icon

Wimbo wa Vijana 1

1
1Vijana wale watatu, Hanania, Mishaeli na Azaria, walitembeatembea katikati ya moto, wakimsifu na kumtukuza Bwana Mungu. 2Kisha, Azaria akasimama katikati ya moto, akaanza kuomba kwa sauti kubwa:
3“Utukuzwe na kusifiwa, ee Bwana, Mungu wa babu zetu!
Jina lako litukuzwe milele.
4Yote uyafanyayo, wayafanya kwa haki kabisa;
matendo yako yote ni mema, njia zako ni sawa,
na hukumu zako zote ni za haki.
5Wewe una haki kuhusu maafa yote uliyosababisha yatupate,
na yaupate Yerusalemu, mji mtakatifu wa babu zetu.
Kwa sababu ya dhambi zetu tuliyastahili yote uliyotuletea.
6Naam, sisi tumekuacha wewe,
tukatenda dhambi, tukavunja sheria zako.
Katika mambo yote sisi tumekukosea sana,
wala hatukuzitii amri zako;
7hatukuyashika hayo,
kama ulivyotuamuru, ili tufanikiwe.
8Basi, yote uliyotuletea,
na yote uliyotutenda,
umeyatenda kwa haki kabisa.
9Umetutia mikononi mwa adui zetu,
watu ambao hawajali sheria,
watu wasiotaka kujua lolote juu ya Mungu;
umetutia mikononi mwa mfalme mbaya,
mfalme mwovu kupita wote ulimwenguni.
10Sasa hatuthubutu hata kulalamika,
aibu na fedheha vimetupata sisi watumishi wako wakuabuduo.
11Kwa ajili ya jina lako, usitutupe kabisa!
Usilitangue agano lako ulilofanya nasi.
12Utuonee huruma,
kwa ajili ya Abrahamu mpendwa wako,
kwa ajili ya Isaka mtumishi wako
na Israeli mtakatifu wako.
13Ukumbuke kwamba uliwapa ahadi,
kwamba wazawa wao watakuwa wengi kama nyota za mbinguni,
naam, wengi kama mchanga wa pwani.
14Maana sasa ee Bwana, tu wachache kuliko mataifa yote;
kwa dhambi zetu twadhulumiwa duniani kote mpaka leo.
15Hatuna tena mfalme, wala nabii, wala kiongozi;
hatuna sadaka za kuteketezwa, wala tambiko, kafara, wala ubani;
hatuna pa kukutolea sadaka na kupata rehema zako.
16Lakini twakujia kwa moyo wa toba na roho ya unyenyekevu,
utukubali kama vile tungekujia na sadaka ya kuteketezwa za kondoo dume na mafahali,
au na maelfu ya wanakondoo wanono.
17Ikubali toba yetu kama sadaka yetu leo,
ili tuweze kukutii kwa moyo wote,
maana, anayekutumaini wewe hataabiki kamwe.
18Sasa twataka kukutii kwa moyo wote;
twataka kukucha na kukutafuta.
19Usikubali tuaibike!
Ututendee kadiri ya uvumilivu wako,
na wingi wa huruma yako!
20Tukomboe kwa matendo yako makuu;
lifanye jina lako kuu litukuke, ee Bwana!
Wote wanaowaudhi watumishi wako waaibishwe.
21Na wafedheheshwe,
na wapokonywe uwezo wao,
nguvu zao na zivunjiliwe mbali;
22wapate kujua kwamba wewe ndiwe Bwana,
ndiwe Mungu peke yako,
mtukufu juu ya ulimwengu wote.”
23Wakati huo wote watumishi wa mfalme ambao waliwatupa hao vijana ndani ya tanuri la moto, walizidisha juhudi zao za kuufanya ule moto uwake kwa ukali zaidi, kwa kumimina humo mafuta na lami, vifuu vya nazi na kuni. 24Hapo, miali ya moto ikapanda juu zaidi ya mita ishirini na tano, 25ikaenea pande zote na kuwateketeza Wakaldayo waliokuwa wamesimama karibu. 26Malaika wa Bwana ambaye alikuwa ameingia katika tanuri pamoja na Azaria na wenzake, aliisukuma kando miali ya moto huo ndani ya tanuri, 27akafanya katikati ya tanuri pawe na upepo wa baridi na unyevunyevu. Kwa hiyo, moto huo haukuwagusa kabisa, wala kuwadhuru, wala kuwasumbua vijana hao.
Wimbo wa Vijana Watatu
28Hapo, wote watatu wakiwa katikati ya tanuri, wakamwimbia Mungu wakamsifu na kumtukuza kwa sauti moja wakisema:
29“Twakusifu ee Bwana, Mungu wa babu zetu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
30Twalisifu jina lako kuu na takatifu;
lastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
31Twakusifu katika hekalu lako la fahari takatifu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
32Twakusifu wewe uketiye juu ya viumbe wenye mabawa na kutazama chini vilindini!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
33Twakusifu ewe uketiaye kiti cha enzi cha ufalme wako!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
34Twakusifu wewe ukaaye katika mawingu ya mbingu!
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele!
35“Msifuni Bwana enyi viumbe vyake vyote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
36Msifuni Bwana enyi mbingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
37Msifuni Bwana enyi malaika wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
38Msifuni Bwana enyi maji yote juu ya mbingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
39Msifuni Bwana enyi wenye mamlaka!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
40Msifuni Bwana enyi jua na mwezi!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
41Msifuni Bwana enyi nyota za mbinguni!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
42Msifuni Bwana mvua yote na ukungu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
43Msifuni Bwana enyi pepo zote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
44Msifuni Bwana enyi moto na joto!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
45Msifuni Bwana enyi kipupwe na hari!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
46Msifuni Bwana enyi umande na theluji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
47Msifuni Bwana enyi usiku na mchana!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
48Msifuni Bwana enyi mwanga na giza!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
49Msifuni Bwana enyi barafu na baridi!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
50Msifuni Bwana enyi ukungu na theluji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
51Msifuni Bwana enyi umeme na mawingu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
52“Dunia na imsifu Bwana!
Imsifu na kumtukuza milele!
53Msifuni Bwana enyi milima na vilima!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
54Msifuni Bwana enyi mimea yote duniani!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
55Msifuni Bwana enyi chemchemi za maji!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
56Msifuni Bwana enyi bahari na mito!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
57Msifuni Bwana enyi nyangumi na viumbe vyote majini!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
58Msifuni Bwana enyi ndege wote wa angani!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
59Msifuni Bwana enyi wanyama wa porini na wafugwao!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
60Msifuni Bwana enyi wanaadamu wote!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
61Msifuni Bwana enyi watu wa Israeli!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
62Msifuni Bwana enyi makuhani wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
63Msifuni Bwana enyi watumishi wake!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
64Msifuni Bwana enyi roho na nafsi za waadilifu!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
65Msifuni Bwana enyi watakatifu na wanyenyekevu wa moyo!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
66Msifuni Bwana enyi Hanania, Azaria na Mishaeli!
Mwimbieni sifa na kumtukuza milele!
Msifuni kwa maana ametuokoa kutoka Kuzimu,
ametuokoa kutoka nguvu za kifo,
ametuokoa ndani ya tanuri la moto mkali;
naam, ametuokoa kutoka katikati ya moto.
67Mshukuruni Bwana kwa maana ni mwema,
kwa maana huruma zake zadumu milele.
68Msifuni enyi mnaomwabudu Bwana, Mungu wa miungu!
Mwimbieni sifa na kumshukuru,
kwa maana huruma zake zadumu milele!”

Currently Selected:

Wimbo wa Vijana 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy