YouVersion Logo
Search Icon

Luka 1

1
1Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. 2Waliyaandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona mambo hayo kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. 3Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, 4ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
Ahadi ya kuzaliwa kwa Yohane
5Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha ukuhani cha Abiya. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. 6Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. 7Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
8Siku moja, ilipokuwa zamu yake kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, 9Zakaria alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. 10Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. 11Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. 12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. 14Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. 16Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. 17Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.”
18Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.” 19Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema. 20Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.”
21Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakaria huku wakishangaa juu ya kukawia kwake hekaluni. 22Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
23Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. 24Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: 25“Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.”
Ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu
26Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu, ewe uliyejaliwa neema na Mungu! Bwana yuko nawe!”
29Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: Maneno hayo yanamaanisha nini? 30Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. 32Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. 36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. 37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” 38Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.
Maria anamtembelea Elisabeti
39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yudea. 40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elisabeti. 41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu, 42akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. 43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44Nakuambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokuambia.”
Utenzi wa Maria
46Naye Maria akasema,
“Moyo wangu wamtukuza Bwana,
47roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu.
Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
49Kwa kuwa Mungu Mwenye Nguvu amenifanyia makuu,
jina lake ni takatifu.
50Huruma yake kwa watu wanaomcha
hudumu kizazi hata kizazi.
51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:
Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi,
akawakweza wanyenyekevu.
53Wenye njaa amewashibisha mema,
matajiri amewaondoa mikono mitupu.
54Amemsaidia Israeli mtumishi wake,
akikumbuka huruma yake,
55kama alivyowaahidia wazee wetu,
Abrahamu na wazawa wake hata milele.”
56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji
57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. 58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. 60Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” 61Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” 62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. 63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. 64Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. 66Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Utenzi wa Zakaria
67Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu:
68“Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli,
kwani amewajia na kuwakomboa watu wake.
69Ametupatia Mwokozi shujaa,
mzawa wa Daudi mtumishi wake.
70Aliahidi hapo kale
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
71kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu
na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
72Alisema atawahurumia wazee wetu,
na kukumbuka agano lake takatifu.
73Alimwapia Abrahamu babu yetu,
kwamba atatujalia sisi
74tukombolewe mikononi mwa maadui zetu,
tupate kumtumikia bila hofu,
75tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake,
siku zote za maisha yetu.
76Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu,
utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
77kuwatangazia watu kwamba wataokolewa
kwa kuondolewa dhambi zao.
78Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma.
Atatuchomozea mwanga kutoka juu,
79na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo,
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.”
80Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.

Currently Selected:

Luka 1: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy