YouVersion Logo
Search Icon

Wagalatia 1

1
1Mimi Paulo niliye mtume si kwa mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu, 2na ndugu wote walio pamoja nami tunayasalimu makanisa ya Galatia. 3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
4Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa. 5Kwake yeye uwe utukufu milele na milele! Amina.
Habari Njema kamili
6Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi Mungu aliyewaita kwa neema ya Kristo, na mnafuata injili ya namna nyingine. 7Lakini hakuna injili nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni injili tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe! 9Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: Kama mtu yeyote anawahubirieni injili ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe!
10Sasa nataka kibali cha nani: Cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo.
Paulo alivyopata wito wake
11Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu. 12Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia.
13Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa. 14Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu.
15Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie. 16Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanawe kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu, 17na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko. 18Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano. 19Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. 20Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo.
21Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia. 22Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea. 23Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: “Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza.” 24Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

Currently Selected:

Wagalatia 1: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy