Methali 16:1-33 BHN

1Binadamu hupanga mipango yake, lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi-Mungu. 2Matendo ya mtu huonekana kwake kuwa sawa, lakini Mwenyezi-Mungu hupima nia ya mtu. 3Mwekee Mwenyezi-Mungu kazi yako, nayo mipango yako itafanikiwa. 4Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake; hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi. 5Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa. 6Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi, kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu. 7Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu, huwageuza hata adui zake kuwa marafiki. 8Afadhali mali kidogo kwa uadilifu, kuliko mapato mengi kwa udhalimu. 9Mtu aweza kufanya mipango yake, lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake. 10Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu; anapotoa hukumu hakosei. 11Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali; mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake. 12Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu, maana msingi wa mamlaka yao ni haki. 13Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu; humpenda mtu asemaye ukweli. 14Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo; mtu mwenye busara ataituliza. 15Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai; wema wake ni kama wingu la masika. 16Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu; kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha. 17Njia ya wanyofu huepukana na uovu; anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake. 18Kiburi hutangulia maangamizi; majivuno hutangulia maanguko. 19Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini, kuliko kugawana nyara na wenye kiburi. 20Anayezingatia mafundisho atafanikiwa; heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu. 21Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili; neno la kupendeza huwavutia watu. 22Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo, bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu. 23Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara; huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia. 24Maneno mazuri ni kama asali; ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya. 25 # Taz Meth 14:12 Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa, lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo. 26Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi, maana njaa yake humsukuma aendelee. 27Mtu mwovu hupanga uovu; maneno yake ni kama moto mkali. 28Mtu mpotovu hueneza ugomvi, mfitini hutenganisha marafiki. 29Mtu mkatili humshawishi jirani yake; humwongoza katika njia mbaya. 30Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu; anayekaza midomo amekwisha nuia mabaya. 31Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu. 32Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu; aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji. 33Kura hupigwa kujua yatakayotukia, lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu.