Parallel
5
Kuomba huruma
1Ukumbuke ee Mwenyezi-Mungu, mambo yaliyotupata!
Utuangalie, uone jinsi tulivyoaibishwa!
2Nchi yetu imekabidhiwa wageni,
nyumba zetu watu wengine.
3Tumekuwa yatima, bila baba,
mama zetu wameachwa kama wajane.
4Maji yetu tunayapata kwa fedha,
kuni zetu kwa kuzinunua.
5Tunalazimishwa kufanya kazi kama punda,
tumechoka lakini haturuhusiwi kupumzika.
6Wamisri na Waashuru tumewanyoshea mikono,
ili tupate chakula cha kutosha.
7Wazee wetu walitenda dhambi na hawapo tena;
nasi tunateseka kwa sababu ya makosa yao.
8Watumwa ndio wanaotutawala,
wala hakuna wa kutuokoa mikononi mwao.
9Chakula chetu twapata kwa kuhatarisha maisha yetu,
maana wauaji wanazurura huko mashambani.
10Ngozi zetu zawaka moto kama tanuri
kwa sababu ya njaa inayotuchoma.
11Wanawake wetu wanashikwa kwa nguvu mjini Siyoni,
binti zetu katika vijiji vya Yuda.
12Wakuu wetu wametungikwa kwa mikono yao;
wazee wetu hawapewi heshima yoyote.
13Vijana wanalazimishwa kusaga nafaka kwa mawe,
wavulana wanayumbayumba kwa mizigo ya kuni.
14Wazee wameacha kutoa mashauri yao,
vijana wameacha kuimba.
15Furaha ya mioyo yetu imetoweka,
ngoma zetu zimegeuzwa kuwa ombolezo.
16Fahari tuliyojivunia imetokomea.
Ole wetu kwa kuwa tumetenda dhambi!
17Kwa ajili hiyo tumeugua moyoni,
kwa mambo hayo macho yetu yamefifia.
18Maana mlima Siyoni umeachwa tupu,
mbweha wanazurura humo.
19Lakini wewe Mwenyezi-Mungu watawala milele,
utawala wako wadumu vizazi vyote.
20Mbona umetuacha muda mrefu hivyo?
Mbona umetutupa siku nyingi hivyo?
21Uturekebishe ee Mwenyezi-Mungu, nasi tukurudie,
uturudishie fahari yetu kama zamani.
22Au, je, umetukataa kabisa?
Je, umetukasirikia mno?