YouVersion Logo
Search Icon

Ezekieli UTANGULIZI

UTANGULIZI
Nabii Ezekieli alitoa huduma yake ya kinabii kuanzia mwaka 593 (taz 1:2) mpaka labda mwaka wa 563 K.K. Mnamo mwaka wa 597 K.K., yeye pamoja na mfalme Yehoyakini na watu mashuhuri wa Yerusalemu, alichukuliwa uhamishoni nchini Babuloni. Ezekieli alitoa mahubiri yake akiwa huko. Mahubiri hayo yaliwahusu hao watu waliohamishwa na wale waliobaki Yerusalemu. Kabla ya kutekwa mji wa Yerusalemu mnamo mwaka wa 586 K.K. mahubiri yake yalihusu hasa kuwaonya watu kuhusu maangamizi ambayo yangetukia baadaye kwa sababu ya dhambi zao; lakini baada ya kutekwa mji wa Yerusalemu, aliwafariji wananchi wenzake, akawapa tumaini la mema ya baadaye. Hivyo ni vipindi viwili ambavyo wengi hubainisha navyo muundo wa mahubiri yake.
Mtindo wa mahubiri yake: Ezekieli alipata mengi ya mahubiri yake ya kinabii katika maono kama tunavyoelezwa katika kitabu chake. Ujumbe wake mara kwa mara unatolewa kwa lugha na matendo yaliyojaa vielelezo na mifano ambayo shabaha yake ni kuonesha umuhimu wa mahubiri hayo. Baadhi ya vielelezo hivyo vyaonekana kwetu kuwa mafumbo na vya kigeni. Hata namna ya kutenda ya Ezekieli mwenyewe ni kielelezo.
1. Nabii Ezekieli anatilia mkazo kwamba, aliongozwa na nguvu kuu ya Mungu na roho yake kutekeleza huduma yake:
a. Mara nyingi kuliko manabii wote anarudiarudia maana hiyo kwa maneno: Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: (Mara 45 kati ya matumizi 60 yanayotumiwa na manabii).
b. Kwa namna ya pekee katika kitabu hiki tuna: Nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu (neno kwa neno: “Mkono wa Mungu ukawa juu yangu”) 1.3; 3.14; 3.22; 33.22; 37.1; 40.1. Msemo ambao una maana ya pekee ya kuchukuliwa au kujazwa nguvu ya kimungu. Mahali pengine katika Biblia maana hiyo inatumika tu katika Yos 4.24; 1 Falme 18.46; Ezra 7.6,8; Luka 1.66; Mate 11.21.
2. Mungu ana mamlaka, anadhibiti na kuona kila kitu ulimwenguni (sura 1). Kwa jumla ujumbe wa maono ya Ezekieli katika sura hii ngumu ni ule wa kuonesha ukuu wake Mungu usiozuilika na uhafifu wa binadamu. Mungu ana mamlaka juu ya ulimwengu wote. Binadamu ni mtu tu, na hata Ezekieli Mungu anamwita “mtu” (neno kwa neno ‘mwana wa mtu’).
3. Nabii pia anatufahamisha kwamba matendo yote ya Mungu yana shabaha maalumu: Watu watambue kuwa yeye ni Mwenyezi-Mungu. Matamshi hayo yanatajwa katika kitabu hiki kwa uchache mara 46 kati ya mara 60 jumla ya matumizi yake katika Biblia yote. Mbali na Ezekieli kitabu cha Kutoka ndicho kinachotumia msemo huo mara nyingi zaidi (mara 7), na hapo inaeleweka kwani kitabu hicho kina ujumbe juu ya tendo kuu la Mungu la kuwaokoa watu wake kutoka Misri. Baada ya kusema hayo na kulinganisha ni dhahiri kwamba huo ni ujumbe mkuu wa Ezekieli, kwamba watu watamtambua Mungu ni Mwenyezi-Mungu. Utambuzi huo sio wa akili bali wa kukiri kuwa yeye ni Mungu mwenye kutenda: Anaadhibu uovu sio tu wa Waisraeli bali pia wa mataifa mengine. Hali kadhalika ni yeye peke yake mwenye kurekebisha na kuwapa uhai (sura 37); mwenye kurekebisha na kusimika uhusiano mpya nao (40–48).
4. Kila mtu atawajibika kwa matendo yake mwenyewe (sura 18). Kila mtu atakufa au kuadhibiwa kwa kosa lake mwenyewe. Taifa linalofuata matakwa ya Mwenyezi-Mungu halitapata adhabu ya dhambi za wazee wake waliotangulia, na kizazi chochote cha baadaye hakitaepa kupata adhabu ati kwa sababu wazee wake waliotangulia walikuwa wema (14.12-23; 18.1-32; 33.1).
Mungu na wachungaji wa watu wa Israeli
Mojawapo ya ujumbe wa pekee wa nabii Ezekieli ni ule unaogusia wadhifa wa viongozi wa watu wa Mungu, sura ya 34 ikiwa hasa ndiyo inayosema juu ya ujumbe huo moja kwa moja. Aliye hasa mchungaji wa watu ni Mungu mwenyewe. Wachungaji wa watu wa Mungu wanatakiwa kushughulikia maslahi ya watu na sio maslahi yao wenyewe. Kutotimiza majukumu yao kutaadhibiwa vikali na wao wenyewe watanyanganywa wadhifa huo. Suala la uchungaji wa watu wa Mungu lipo pia katika manabii wengine na jambo la kumfananisha Mungu na mchungaji mwema wa kondoo ni mojawapo ya vielelezo muhimu sana katika Biblia.
Kitabu chenyewe chagawanyika katika sehemu mbili kuu:
1. Sura 1–32 Yahusu kipindi cha kwanza kabla ya kuteketezwa hekalu na mji wa Yerusalemu. Katika kipindi hiki, sura 4–24, nabii anawakabili watu wa Israeli kuhusu maovu yao hasa ya utovu wa uaminifu kwa Mungu wao (6:13; 16.20; 20.23-28; 23.37-38). Vilevile anawakaripia kwa sababu ya ukosefu wa maisha adili na dhambi za uvunjaji wa haki na ulanguzi (22.11-12). Kwa wingi hukumu zinazotangazwa katika sura 25–32 dhidi ya mataifa mengine zilitolewa pia katika kipindi hiki cha kwanza na nyingine katika kipindi cha pili. Hayo mataifa mengine yanatangaziwa adhabu kwa ufisadi wao na kwa kuwadhulumu watu wa Israeli.
2. Sura 33–48 Karibu mambo yote katika sehemu hii yanahusikana na kipindi cha pili cha huduma ya nabii. Kwa jumla sehemu hii inashughulikia kuwatia moyo wale Waisraeli walioathirika kwa kitendo cha kupelekwa uhamishoni na kwa tukio la kuteketezwa hekalu na mji wa Yerusalemu. Watu wanapewa matumaini (33–39). Kisha, katika 40–48 tuna maono aliyojaliwa nabii kuhusu kuweko tena kwa Mwenyezi-Mungu hekaluni Yerusalemu, kati ya watu wake ambao pia wanagawanyiwa upya nchi yao. Kitabu kinaishia kwa maneno mazito: Jina la mjilitakuwa “Mwenyezi-Mungu Yupo Hapa.” Yafaa lakini kukumbuka kwamba ahadi za Mungu za kuwapa nafuu watu wake na kuwarudishia uhusiano mwema naye zinapatikana pia mahali pengine pia katika sehemu ya kipindi cha kwanza: “Moyo mpya” (k.m. 11.17-20), lakini kwa jumla hapa ndipo hasa wazo hilo linapozingatiwa zaidi.

Currently Selected:

Ezekieli UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy