1 Wakorintho UTANGULIZI
UTANGULIZI
Barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakristo wa Korintho iliandikwa na Paulo mnamo mwaka wa 54 B.K. huko Efeso wakati wa ziara yake ya tatu ya kuhubiri Habari Njema. Mji wa Korintho ulikuwa maarufu katika nchi ya Ugiriki nyakati hizo. Ulikuwa mji wa biashara na maarufu kwa utamaduni. Huko kulikuwa na ibada za miungu mbalimbali. Kama ilivyo kawaida ya miji, Korintho kulikuwa na matatizo yote ya maisha ya mjini. Wakristo wa Korintho pia walijikuta wakishiriki matatizo hayo ya maisha ya mjini. Paulo alikuwa ameanzisha huko Korintho jumuiya ya wafuasi wa Kristo, yaani Wakristo, wakati wa ziara yake ya pili ya kuhubiri Habari Njema. Wakati huo alikaa huko Korintho mwaka mmoja na nusu.
Barua hii iliandikwa kutoa mwongozo juu ya masuala mbalimbali ambayo Paulo alikuwa ameyapokea kutoka kwa jumuiya hiyo ya Korintho (tazama 7:1). Kulingana na 5:9, Paulo alikuwa amekwisha andika barua nyingine lakini kwa bahati mbaya barua hiyo haikuhifadhiwa. Paulo anayakabili masuala ya namna kadhaa ambayo yalihusu Wakristo wa Korintho na kuyajibu au kutoa mawaidha yake. Kati ya hayo ni uhusiano wa jumuiya ya Wakristo na jirani zao wasioamini.
Sura 1–6 – Paulo anataja na kutatua tatizo la maisha mabaya katika kanisa, mgawanyiko miongoni mwao na kushtakiana katika mahakama za wasioamini.
Sura 7–10 – zinashughulikia maswali ya jumla, na sio masuala kutoka kwa Wakristo wa Korintho peke yao: Juu ya kuoa, na juu ya vyakula.
Sura 11–14 – baada ya Paulo kujibu maswali ya sura zilizotangulia anazungumzia juu ya kukutana pamoja kama Wakristo, kuadhimisha Karamu ya Bwana, na juu ya kupokea vipaji mbalimbali vya kiroho katika jumuiya.
Sura 15–16 – zinazungumzia ufufuo wa Kristo na wa waumini. Hapa napo pana mawaidha juu ya kuwa na mpango katika jumuiya ya Wakristo.
Currently Selected:
1 Wakorintho UTANGULIZI: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.