YouVersion Logo
Search Icon

Tobiti 1

1
1Hizi ni habari za maisha ya Tobiti mwana wa Tobieli, mwana wa Ananieli, mwana wa Adueli, mwana wa Gabaeli, wa ukoo wa Asieli, wa kabila la Naftali. 2Wakati Shalmanesa alipokuwa mfalme wa Ashuru, Tobiti alichukuliwa uhamishoni kutoka mji wa Thisbe ulioko kusini mwa Kadeshi huko Naftali kaskazini mwa Galilaya, magharibi-kaskazini mwa mji wa Hazori na kaskazini mwa Shefati.
Maisha ya ujana ya Tobiti
3Mimi Tobiti nimefuata njia za haki na kutenda mema maisha yangu yote. Mara nyingi niliwasaidia jamaa na Wayahudi wenzangu maskini waliohamishiwa pamoja nami huko Ninewi, nchini Ashuru. 4Nilipokuwa kijana nikiwa bado nyumbani nchini Israeli, makabila yote katika Israeli yaliwajibika kwenda kutoa sadaka Yerusalemu. Yerusalemu ulikuwa ndio mji pekee ambao Mungu alikuwa ameuteua miongoni mwa miji yote ya Israeli uwe mahali pa kutolea tambiko zao; huko ndiko kulikojengwa hekalu ambalo ni makao yake matakatifu na ya kudumu. Lakini kabila langu lote la Naftali lilijitenga na mji wa Yerusalemu na ukoo wa Daudi. 5Ndugu zangu wote na ukoo wa Naftali walitambikia juu ya kila kilima kwa ile sanamu ya ndama aliyoifanya Yeroboamu mfalme wa Israeli huko Dani katika mkoa wa Galilaya.
Tobiti azingatia dini yake
6Katika jamaa yangu ni mimi peke yangu niliyekwenda kuabudu mara kwa mara huko Yerusalemu kutekeleza sheria inayowabana watu wote wa Israeli milele. Niliharakisha kwenda Yerusalemu na sehemu ya mazao ya kwanza ya mavuno na wanyama, zaka za mifugo na manyoya ya kwanza ya kondoo. 7Vitu hivi niliwapa makuhani, wazawa wa Aroni, kwa ajili ya madhabahu. Niliwapa Walawi waliohudumu huko Yerusalemu zaka yangu ya divai, ngano, zeituni, makomamanga na matunda mengine. Kwa miaka sita#1:7 miaka sita: Mwaka wa saba ardhi ilipumzishwa na kwa sababu hiyo hayakuwako mavuno. mfululizo nilichukua fedha ya zaka na kuilipa huko Yerusalemu. 8Sehemu ya tatu ya zaka niliwapa yatima, wajane na wageni walioishi miongoni mwa watu wa Israeli; niliwapelekea kama zawadi kila miaka mitatu. Tulipokula chakula tulifanya kulingana na Sheria ya Mose na mawaidha ya Debora mama wa babu yangu Ananieli. Baba yangu alikuwa amekufa akaniacha yatima.
Uaminifu wa Tobiti uhamishoni
9Mara nilipokuwa mtu mzima nilimwoa Ana, mwanamke wa kabila langu. Tulijaliwa mtoto tukamwita Tobia. 10Baadaye nilichukuliwa mateka na kupelekwa Ninewi.
Tulipokuwa tunakaa Ninewi jamaa zangu na Wayahudi wenzangu wote walikuwa wakila chakula walichokula wale watu wasio Wayahudi, 11lakini mimi nilikataa kula chakula hicho. 12Kwa kuwa nilizishika kwa moyo amri za Mungu aliye juu, 13Mungu alimfanya mfalme Shalmanesa anipendelee na kunijali, hata nikapewa madaraka ya kumnunulia mfalme chakula chake.
14Kabla mfalme huyo hajafariki, nilikwenda mara nyingi nchini Media kumnunulia vitu. Siku moja, nilipokuwa mjini Rage huko Media, nilimwachia Gabaeli, nduguye Gabria, fedha mifuko kadhaa, nikamwomba anitunzie. Ndani ya mifuko hiyo mlikuwa na sarafu za shaba zaidi ya kilo 300. 15Shalmanesa alipofariki, Senakeribu, mwanawe, alitawala mahali pake. Mara yakazuka majambazi huko na huko katika barabara za Media, nami nikashindwa kwenda tena Media.
Tobiti azika wafu
16Shalmanesa alipokuwa bado anatawala, niliwasaidia sana Wayahudi wenzangu maskini. 17Wenye njaa, niliwapatia chakula changu na kuwapa nguo wale waliotindikiwa nazo. Kila nilipokuta maiti ya mmoja wa watu wangu ametupwa nje ya ukuta wa mji, nilimwokota na kumzika kwa heshima.
18Mfalme Senakeribu alipomuua mtu yeyote aliyekimbilia nchini mwake kutoka Yudea, mimi nilimzika kwa siri. Mfalme aliwaua watu wengi kutuliza hasira yake. Baadaye alipozitafuta maiti hizo hakuzipata.
19Halafu mtu mmoja wa Ninewi alimwarifu mfalme kwamba mimi ndiye niliyekuwa nikiwazika Waisraeli waliouawa. Nilipogundua kuwa mfalme alipata kujua habari zangu zote, na nilipoona mimi mwenyewe watu wakinitafuta kuniua niliingiwa na hofu na kutoroka. 20Mali yangu yote ikataifishwa na kuwekwa katika hazina ya mfalme. Nilibakiwa tu na mke wangu Ana na mwanangu Tobia.
Tobiti aokolewa na binamu yake
21Ilipokuwa bado hata hazijapita siku hamsini wana wawili wa Senakeribu walimuua baba yao, wakakimbilia kwenye milima ya Ararati. Esar-hadoni, mwana mwingine wa Senakeribu, akawa mfalme; akamteua Ahika, mwana wa ndugu yangu Anaeli, awe waziri wa fedha na mratibu wa mambo yote ya utawala. 22Basi, Ahika alinitetea, nikaruhusiwa kurudi Ninewi. Hii ilikuwa mara ya pili Ahika kuwa na cheo hicho, maana alikwisha kuwa mhudumu mkuu wa divai, waziri wa fedha, mhasibu na mwangalizi wa mhuri wa ofisi chini ya mfalme Senakeribu, naye Esar-hadoni akamthibitisha katika madaraka hayo. Ahika alikuwa binamu yangu.

Currently Selected:

Tobiti 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy