YouVersion Logo
Search Icon

Yeremia 1

1
1Yafuatayo ni maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani wa mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini. 2Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda. 3Lilimjia tena wakati Yehoyakimu mwana wa Yosia, alipokuwa mfalme wa Yuda. Yeremia aliendelea kupata neno la Mwenyezi-Mungu hadi mwishoni mwa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Mnamo mwezi wa tano wa mwaka huo, watu wa Yerusalemu walipelekwa uhamishoni.
Yeremia anaitwa kuwa nabii
4Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake:
5“Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua,
kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu;
nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.”
6Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu,
mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana.
7Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia,
“Usiseme kwamba wewe ni kijana bado.
Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao,
na yote nitakayokuamuru utayasema.
8Wewe usiwaogope watu hao,
kwa maana niko pamoja nawe kukulinda.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
9Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia,
“Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako.
10Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme,
uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa,
mamlaka ya kuharibu na kuangamiza,
mamlaka ya kujenga na ya kupanda.”
Maono mawili
11Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi#1:11 mlozi: Mti wa kwanza kuchanua baada ya mvua nchini Palestina; aidha hapa tunapewa picha ya mti ambao ulikuwa “macho” tayari kuchanua mara baada ya mvua. unaochanua.” 12Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.”
13Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.”
14Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii. 15Maana naziita falme zote za kaskazini na makabila yote. Wafalme wake wote watakuja na kila mmoja wao ataweka kiti chake cha enzi mbele ya malango ya Yerusalemu na kandokando ya kuta zake zote, na kuizunguka miji yote ya Yuda. 16Nami nitawahukumu Waisraeli kwa ajili ya uovu wao wote wa kuniacha mimi, wakafukizia ubani miungu mingine na kuabudu sanamu walizojitengenezea wenyewe. 17Sasa basi, wewe Yeremia jiweke tayari. Haya! Nenda ukawaambie mambo yote ninayokuamuru. Usiwaogope, nisije nikakufanya mwoga mbele yao. 18Leo hii nakufanya kuwa imara kama mji uliozungukwa na ngome, kama mnara wa chuma na kama ukuta wa shaba nyeusi, dhidi ya nchi yote, dhidi ya wafalme wa Yuda, wakuu wake, makuhani wake na watu wake wote. 19Watapigana nawe, lakini hawatashinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Currently Selected:

Yeremia 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy