YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 89:1-18

Zaburi 89:1-18 BHND

Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele; nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako. Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele; uaminifu wako ni thabiti kama mbingu. Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi: ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme, tena nitaudumisha ufalme wako milele.’” Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu; uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu. Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu? Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni? Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu; wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu? Uaminifu umekuzunguka pande zote. Wewe watawala machafuko ya bahari; mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza. Uliliponda joka Rahabu na kuliua; uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako. Mbingu ni zako na dunia ni yako pia; ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba. Wewe uliumba kaskazini na kusini; milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha. Mkono wako una nguvu, mkono wako una nguvu na umeshinda! Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako; fadhili na uaminifu vyakutangulia! Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako. Wewe ndiwe fahari na nguvu yao; kwa wema wako twapata ushindi. Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako, mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli.

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy