YouVersion Logo
Search Icon

Luka 19

19
Yesu na Zakayo
1Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake. 2Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. 3Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. 4Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. 5Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. 6Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. 7#Lk 15:2 Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. 8#Kut 22:1; Hes 5:6,7 Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. 9#Lk 13:16; Mdo 3:25; 16:31 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Abrahamu. 10#Mt 18:11; Eze 34:16; Yn 3:17; Lk 5:32; 1 Tim 1:15 Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
Mfano wa mafungu kumi ya fedha
11 # Mt 25:14-30 Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara moja. #Lk 24:21; Mdo 1:6 12#Mk 13:34 Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. 13Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hadi nitakaporudi. 14#Yn 1:11 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. 15Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. 16Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. 17#Lk 16:10 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. 18Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida. 19Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. 20Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka salama katika kitambaa. 21Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; wachukua usichoweka, wavuna usichopanda. 22Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, nichukuaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; 23basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? 24Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. 25Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi. 26#Mt 13:12; Mk 4:25; Lk 8:18 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho. 27Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa muwachinje mbele yangu.
Yesu aingia Yerusalemu kwa shangwe
28Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.
29 # Mt 21:1-9; Mk 11:1-10; Yn 12:12-16 Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, 30akisema, Nendeni mpaka katika kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwanapunda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu yeyote bado, mfungueni mkamlete hapa. 31Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. 32Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. 33Na walipokuwa wakimfungua mwanapunda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwanapunda? 34Wakasema, Bwana anamhitaji. 35Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwanapunda, wakampandisha Yesu. 36#2 Fal 9:13 Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. 37Na alipokuwa amekaribia mteremko wa mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, 38#Zab 118:26; Lk 2:14 wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. 39Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. 40Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatanena kwa sauti kuu.
Yesu aulilia Yerusalemu
41 # 2 Fal 8:11; Yn 11:35 Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, 42#Kum 32:29; Mt 13:14; Yn 12:38 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. 43Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; 44#Lk 21:6; Zab 137:9 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiwa kwako.
Yesu atakasa hekalu
45 # Mt 21:12-16; Mk 11:15-18; Yn 2:13-16 Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, 46#Isa 56:7; Yer 7:11 akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.
47 # Lk 21:37; 22:53; Yn 18:20 Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; 48wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.

Currently Selected:

Luka 19: SRUVDC

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy