Zab 119
SUV

Zab 119

119
Utukufu wa Sheria ya Mungu
1 # Zab 128:1 Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya BWANA.
2 # Kum 4:29 Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
3 # Rum 7:16,17; 1 Yoh 3:9 Naam, hawakutenda ubatili,
Wamekwenda katika njia zake.
4Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
5 # Yer 31:33; Rum 7:22,23; 2 Kor 3:5 Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako.
6 # Ayu 22:26; 1 Yoh 2:28 Ndipo mimi sitaaibika,
Nikiyaangalia maagizo yako yote.
7Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako
8Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa
* * *
9 # Mit 1:4,10 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?
Kwa kutii, akilifuata neno lako.
10 # 2 Nya 15:15 Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
11 # Lk 2:19 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi.
12Ee BWANA, umehimidiwa,
Unifundishe amri zako.
13Kwa midomo yangu nimezisimulia
Hukumu zote za kinywa chako.
14Nimeifurahia njia ya shuhuda zako
Kana kwamba ni mali mengi.
15 # Zab 1:2 Nitayatafakari mausia yako,
Nami nitaziangalia njia zako.
16Nitajifurahisha sana kwa amri zako,
Sitalisahau neno lako.
* * *
17Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
18Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako.
19 # Mwa 47:9; Ebr 11:13 Mimi ni mgeni katika nchi,
Usinifiche maagizo yako.
20Roho yangu imepondeka kwa kutamani
Hukumu zako kila wakati.
21Umewakemea wenye kiburi,
Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
22Uniondolee laumu na dharau,
Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
23Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
24Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
* * *
25 # Zab 143:11 Nafsi yangu imeambatana na mavumbi,
Unihuishe sawasawa na neno lako.
26 # 1 Fal 8:36; Zab 27:11 Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundishe amri zako.
27Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
28Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
29 # Mit 30:8; Ebr 8:10 Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
30Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
31Nimeambatana na shuhuda zako,
Ee BWANA, usiniaibishe.
32 # 1 Fal 4:29; Isa 60:5; 2 Kor 6:11 Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako,
Utakaponikunjua moyo wangu.
* * *
33 # Mt 10:22; Ufu 2:26 Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako,
Nami nitaishika hata mwisho.
34 # Mit 2:6; Yak 1:5 Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
35Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
36 # Eze 33:31; Mk 7:21; Lk 12:15; 1 Tim 6:10; Ebr 13:5 Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako,
Wala usiielekee tamaa.
37 # Ayu 31:1 Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,
Unihuishe katika njia yako.
38 # 2 Sam 7:25 Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako,
Inayohusu kicho chako.
39Uniondolee laumu niiogopayo,
Maana hukumu zako ni njema.
40Tazama, nimeyatamani mausia yako,
Unihuishe kwa haki yako.
* * *
41Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi,
Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
42Nami nitamjibu neno anilaumuye,
Kwa maana nalitumainia neno lako.
43Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe,
Maana nimezingojea hukumu zako.
44Nami nitaitii sheria yako daima,
Naam, milele na milele.
45 # Yn 8:32,36; Rum 8:2 Nami nitakwenda panapo nafasi,
Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
46 # Mt 10:18; Mdo 26:1,2 Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme,
Wala sitaona aibu.
47Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,
Ambayo nimeyapenda.
48Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda,
Nami nitazitafakari amri zako.
* * *
49Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako,
Kwa sababu umenitumainisha.
50 # Zab 27:13; Yer 15:16; Rum 5:3-5; Ebr 6:17-19 Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu,
Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.
51 # Yer 20:7; Ayu 23:11 Wenye kiburi wamenidharau mno,
Sikujiepusha na sheria zako.
52Nimezikumbuka hukumu zako za kale,
Ee BWANA, nikajifariji.
53 # Ezr 9:3 Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
54Amri zako zimekuwa nyimbo zangu,
Katika nyumba ya ugeni wangu.
55 # Zab 63:6 Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako,
Ee BWANA, nikaitii sheria yako.
56Hayo ndiyo niliyokuwa nayo,
Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
* * *
57 # Zab 16:5; Yer 10:16; Omb 3:24 BWANA ndiye aliye fungu langu,
Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.
58Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote,
Unifadhili sawasawa na ahadi yako.
59 # Omb 3:40; Yoe 2:13; Lk 15:17 Nalizitafakari njia zangu,
Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.
60Nalifanya haraka wala sikukawia,
Kuyatii maagizo yako.
61Kamba za wasio haki zimenifunga,
Sikuisahau sheria yako.
62 # Mdo 16:25 Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru,
Kwa sababu ya hukumu zako za haki.
63Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao,
Na wale wayatiio mausia yako.
64 # Zab 33:5 BWANA, dunia imejaa fadhili zako,
Unifundishe amri zako.
* * *
65Umemtendea mema mtumishi wako,
Ee BWANA, sawasawa na neno lako.
66Unifundishe akili na maarifa,
Maana nimeyaamini maagizo yako.
67 # Kum 32:15; Yer 31:18; Hos 5:15; Ebr 12:11; Ufu 3:19 Kabla sijateswa mimi nalipotea,
Lakini sasa nimelitii neno lako.
68 # Kut 34:6; Zab 107:1; Mt 19:7 Wewe U mwema na mtenda mema,
Unifundishe amri zako.
69 # Ayu 13:4 Wenye kiburi wamenizulia uongo,
Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.
70 # Mdo 28:27 Mioyo yao imenenepa kama shahamu,
Mimi nimeifurahia sheria yako.
71 # Ebr 12:10; Mit 8:10 Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
Nipate kujifunza amri zako.
72Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
* * *
73 # Ayu 10:8; Zab 100:3 Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza,
Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.
74 # Zab 34:2 Wakuchao na wanione na kufurahi,
Kwa sababu nimelingojea neno lako.
75 # Zab 89:30-33; Ebr 12:10 Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa.
76Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
77Rehema zako zinijie nipate kuishi,
Maana sheria yako ni furaha yangu.
78 # Zab 25:3 Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo,
Mimi nitayatafakari mausia yako.
79Wakuchao na wanirudie,
Nao watazijua shuhuda zako.
80 # 2 Nya 15:7; Mit 4:23; Yn 1:47 Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako,
Nisije mimi nikaaibika.
* * *
81 # Zab 42:1,2; 73:26 Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako,
Nimelingojea neno lako.
82 # Zab 69:3 Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako,
Nisemapo, Lini utakaponifariji?
83 # Ayu 30:30 Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi,
Sikuzisahau amri zako.
84 # Zab 39:4; 7:6; Ufu 6:10 Siku za mtumishi wako ni ngapi,
Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?
85 # Zab 35:7 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo,
Ambao hawaifuati sheria yako.
86 # Zab 7:1-5; 35:19 Maagizo yako yote ni amini,
Wananifuatia bure, unisaidie.
87Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi,
Lakini sikuyaacha mausia yako.
88Unihuishe kwa fadhili zako,
Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
* * *
89 # Mt 5:18; 1 Pet 1:25 Ee BWANA, neno lako lasimama
Imara mbinguni hata milele.
90Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi,
Umeiweka nchi, nayo inakaa.
91 # Mwa 8:22; Zab 148:6; Yer 33:25 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 # Rum 15:4 Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu,
Hapo ningalipotea katika taabu zangu.
93Hata milele sitayasahau maagizo yako,
Maana kwa hayo umenihuisha.
94 # Hos 2:7,16 Mimi ni wako, uniokoe,
Kwa maana nimejifunza mausia yako.
95Wasio haki wameniotea ili kunipoteza,
Nitazitafakari shuhuda zako.
96 # Isa 40:8; Mt 5:18 Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho,
Bali agizo lako ni pana mno.
* * *
97 # Zab 1:2 Sheria yako naipenda mno ajabu,
Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
98 # Kum 4:6,8; Isa 48:17 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu,
Kwa maana ninayo sikuzote.
99 # 2 Tim 3:15 Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote,
Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
100 # Ayu 12:12; 32:7 Ninao ufahamu kuliko wazee,
Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.
101 # 2 Kor 7:1; Mit 1:15 Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako.
102Sikujiepusha na hukumu zako,
Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.
103 # Zab 19:10; Mit 8:11 Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asali kinywani mwangu.
104Kwa mausia yako najipatia ufahamu,
Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
* * *
105Neno lako ni taa ya miguu yangu,
Na mwanga wa njia yangu.
106 # Neh 10:29 Nimeapa nami nitaifikiliza,
Kuzishika hukumu za haki yako.
107Nimeteswa mno;
Ee BWANA, unihuishe sawasawa na neno lako.
108 # Hos 14:2; Ebr 13:15 Ee BWANA, uziridhie sadaka za kinywa changu,
Na kunifundisha hukumu zako.
109 # Amu 12:3; Ayu 13:14 Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima,
Lakini sheria yako sikuisahau.
110Watendao uovu wamenitegea mtego,
Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.
111 # Kum 33:4 Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
112Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako,
Daima, naam, hata milele.
* * *
113Watu wa kusita-sita nawachukia,
Lakini sheria yako naipenda.
114 # Zab 32:7 Ndiwe sitara yangu na ngao yangu,
Neno lako nimelingojea.
115 # Zab 6:8; Mt 7:23 Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu,
Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
116 # Zab 25:2; Rum 5:5; 9:33 Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi,
Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
117 # Zab 71:6; Yn 10:28; Rum 14:4 Unisaidie nami nitakuwa salama,
Nami nitaziangalia amri zako daima.
118Umewakataa wote wazikosao amri zako,
Kwa maana hila zao ni uongo.
119 # Eze 22:18 Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka,
Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
120 # Hab 3:16 Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe,
Nami ninaziogopa hukumu zako.
* * *
121Nimefanya hukumu na haki,
Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
122 # Ebr 7:22 Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema,
Wenye kiburi wasinionee.
123Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako,
Na ahadi ya haki yako.
124Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako,
Na amri zako unifundishe.
125Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,
Nipate kuzijua shuhuda zako.
126Wakati umewadia BWANA atende kazi;
Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
127 # Zab 19:10; Efe 3:8; Mit 3:13,18; 8:11 Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako,
Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
128Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili,
Kila njia ya uongo naichukia.
* * *
129Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
130 # Zab 19:11; Mit 1:4; 2 Pet 1:19 Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
131Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
132 # Kut 4:31; 1 Sam 1:11; Zab 106:4 Unigeukie, unirehemu mimi,
Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.
133 # Rum 6:12 Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,
Uovu usije ukanimiliki.
134 # Lk 1:74 Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu,
Nipate kuyashika mausia yako.
135 # Zab 4:6 Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
136 # Yer 9:1 Macho yangu yachuruzika mito ya maji,
Kwa sababu hawaitii sheria yako.
* * *
137 # Neh 9:33; Yer 12:1; Dan 9:7 Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki,
Na hukumu zako ni za adili.
138Umeziagiza shuhuda zako kwa haki,
Na kwa uaminifu mwingi.
139Juhudi yangu imeniangamiza,
Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.
140Neno lako limesafika sana,
Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.
141 # Mit 15:16; Amo 7:2; Lk 6:20; 2 Kor 8:9; Yak 2:5 Mimi ni mdogo, nadharauliwa,
Lakini siyasahau mausia yako.
142 # Zab 19:9; Yn 17:17; Efe 1:13 Haki yako ni haki ya milele,
Na sheria yako ni kweli.
143Taabu na dhiki zimenipata,
Maagizo yako ni furaha yangu.
144Haki ya shuhuda zako ni ya milele,
Unifahamishe, nami nitaishi.
* * *
145Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee BWANA, uitike;
Nitazishika amri zako.
146Nimekuita Wewe, uniokoe,
Nami nitazishika shuhuda zako.
147Kutangulia mapambazuko naliomba msaada,
Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.
148 # Zab 63:1,6 Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku,
Ili kuitafakari ahadi yako.
149Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako,
Ee BWANA, unihuishe sawasawa na hukumu yako.
150Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
Wamekwenda mbali na sheria yako.
151 # Zab 145:18 Ee BWANA, Wewe U karibu,
Na maagizo yako yote ni kweli.
152 # Lk 21:33 Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako,
Ya kuwa umeziweka zikae milele.
* * *
153 # Omb 5:1 Uyaangalie mateso yangu, uniokoe,
Maana sikuisahau sheria yako.
154 # 1 Sam 24:15; Zab 35:1; Mik 7:9 Unitetee na kunikomboa,
Unihuishe sawasawa na ahadi yako.
155 # Ayu 5:4 Wokovu u mbali na wasio haki,
Kwa maana hawajifunzi amri zako.
156Ee BWANA, rehema zako ni nyingi,
Unihuishe sawasawa na hukumu zako.
157Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi,
Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.
158Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
Kwa sababu hawakulitii neno lako.
159Uangalie niyapendavyo mausia yako,
Ee BWANA, unihuishe sawasawa na fadhili zako.
160Jumla ya neno lako ni kweli,
Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
* * *
161 # 1 Sam 24:11 Wakuu wameniudhi bure,
Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.
162Naifurahia ahadi yako,
Kama apataye mateka mengi.
163Nimeuchukia uongo, umenikirihi,
Sheria yako nimeipenda.
164Mara saba kila siku nakusifu,
Kwa sababu ya hukumu za haki yako.
165 # Mit 3:2; Isa 32:17 Wana amani nyingi waipendao sheria yako,
Wala hawana la kuwakwaza.
166Ee BWANA, nimeungojea wokovu wako,
Na maagizo yako nimeyatenda.
167Nafsi yangu imezishika shuhuda zako,
Nami nazipenda mno.
168 # Ayu 34:21; Mit 5:21 Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako,
Maana njia zangu zote zi mbele zako.
* * *
169Ee BWANA, kilio changu na kikukaribie,
Unifahamishe sawasawa na neno lako.
170Dua yangu na ifike mbele zako,
Uniponye sawasawa na ahadi yako.
171Midomo yangu na itoe sifa,
Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.
172Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako,
Maana maagizo yako yote ni ya haki.
173 # Yos 24:22; Mit 1:29; Lk 10:42 Mkono wako na uwe tayari kunisaidia,
Maana nimeyachagua mausia yako.
174Ee BWANA, nimeutamani wokovu wako,
Na sheria yako ndiyo furaha yangu.
175Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,
Na hukumu zako zinisaidie.
176 # Isa 53:6; Mt 10:6; Lk 15:4; 1 Pet 2:25; Eze 34:6; Mt 18:11 Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea;
Umtafute mtumishi wako;
Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.


Learn More About Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia

Encouraging and challenging you to seek intimacy with God every day.


YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy.