YouVersion Logo
Search Icon

Yohana 14

14
Yesu Awatia Moyo Wanafunzi Wake
1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”
Yesu Ndiye Njia Ya Kwenda Kwa Baba
5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”
6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. 7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”
8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”
9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12 Amin, amin nawaambia, yeyote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.
Yesu Aahidi Roho Mtakatifu
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. 18 Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu. 19 Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. 20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu. 21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”
23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.
“Haya inukeni; twendeni zetu.

Currently Selected:

Yohana 14: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy